Agano la Kale

Agano Jipya

Kutoka 8:22-30 Biblia Habari Njema (BHN)

22. Lakini siku hiyo sehemu ya Gosheni wanakoishi watu wangu nitaikinga: Humo nzi hao hawatakuwamo. Hapo ndipo utakapotambua kwamba mimi Mwenyezi-Mungu natenda mambo nchini mwako.

23. Nitawakinga watu wangu na mambo yatakayowapata watu wako. Mambo hayo yatafanyika kesho.’”

24. Mwenyezi-Mungu akafanya kama alivyosema: Makundi makubwa ya nzi yakaivamia nyumba ya Farao, nyumba za maofisa wake na nchi nzima ya Misri. Nchi nzima ya Misri ikaharibiwa na nzi hao.

25. Ndipo Farao akawaita Mose na Aroni, akasema, “Mnaweza kwenda kumtambikia Mungu wenu, lakini iwe humuhumu nchini Misri.”

26. Lakini Mose akamjibu, “La! Haifai kufanya hivyo, maana tambiko tutakazomtolea Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, zitawachukiza Wamisri. Je, Wamisri wakituona tukitoa tambiko ambazo ni chukizo kwao, si watatupiga mawe?

27. Ni lazima tusafiri mwendo wa siku tatu jangwani tukamtambikie Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, kama atakavyotuamuru.”

28. Basi, Farao akasema, “Nitawaacha mwende zenu kumtambikia Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, jangwani. Walakini msiende mbali mno. Niombeeni na mimi.”

29. Mose akamjibu, “Mara tu nitakapokuacha, nitamwomba Mwenyezi-Mungu makundi haya ya nzi yatoweke kwako wewe Farao, maofisa wako na watu wako, kesho. Lakini wewe usitudanganye tena kwa kukataa kuwaacha watu kwenda kumtambikia Mwenyezi-Mungu.”

30. Basi, Mose akaondoka nyumbani kwa Farao, akamwomba Mwenyezi-Mungu.

Kusoma sura kamili Kutoka 8