Agano la Kale

Agano Jipya

Kutoka 5:12-23 Biblia Habari Njema (BHN)

12. Basi, watu wote wakatawanyika kila mahali nchini Misri wakitafuta nyasi za kutengenezea matofali.

13. Nao Wanyapara wakakazana wakisema, “Timizeni kazi yenu ya kila siku kama hapo awali mlipoletewa nyasi.”

14. Wanyapara Wamisri wakawapiga wasimamizi wa Waisraeli waliochaguliwa kusimamia kazi wakisema, “Kwa nini hamtimizi kazi yenu na kufikisha idadi ileile ya matofali kama awali?”

15. Ndipo wasimamizi wa Waisraeli walipomwendea Farao, wakamlilia wakisema, “Kwa nini unatutenda hivi sisi watumishi wako?

16. Hatupewi tena nyasi zozote na huku tunalazimishwa kufyatua matofali. Tena sisi watumishi wako tunapigwa, hali kosa ni la watu wako.”

17. Lakini Farao akasema, “Wavivu nyinyi; nyinyi ni wavivu, ndio maana mnasema, ‘Tuache twende tukamtambikie Mwenyezi-Mungu’.

18. Nendeni sasa mkafanye kazi; maana hamtapewa nyasi zozote na mtafyatua idadi ileile ya matofali.”

19. Basi, hao wasimamizi wa Waisraeli sasa walijiona kuwa wako taabuni, kwani waliambiwa, “Hamtaipunguza kamwe idadi ya matofali ya kila siku.”

20. Walipoondoka kwa Farao, walikutana na Mose na Aroni ambao walikuwa wanawangojea.

21. Basi, wakawaambia Mose na Aroni, “Mwenyezi-Mungu na aone jambo hili na kuwahukumu nyinyi kwa sababu mmetufanya sisi kuwa chukizo kwa Farao na maofisa wake; nyinyi mmewapa sababu ya kutuua.”

22. Kisha Mose akamgeukia tena Mwenyezi-Mungu, akasema, “Ee Mwenyezi-Mungu, kwa nini unawatendea watu hawa uovu? Kwa nini hata ulinituma?

23. Tangu nilipokwenda na kuongea na Farao kwa jina lako, yeye amewatendea uovu watu hawa. Wewe hujafanya lolote kuwakomboa watu wako.”

Kusoma sura kamili Kutoka 5