Agano la Kale

Agano Jipya

Kutoka 40:20-36 Biblia Habari Njema (BHN)

20. Kisha alichukua vile vibao viwili vya mawe na kuviweka katika lile sanduku. Aliipitisha ile mipiko katika vikonyo vya sanduku na kukiweka kiti cha rehema juu yake.

21. Kisha akaliweka lile sanduku la maamuzi ndani ya hema na kutundika pazia, na kwa namna hiyo akalisitiri sanduku la maamuzi, kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu.

22. Aliweka meza ndani ya hema la mkutano, upande wa kaskazini, sehemu ya nje ya pazia,

23. na juu yake akaipanga mikate iliyotolewa kwa Mwenyezi-Mungu, kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu.

24. Alikiweka kinara ndani ya hema la mkutano, upande wa kusini, mkabala wa meza.

25. Humo, mbele ya Mwenyezi-Mungu, akaziwasha taa zake, kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu.

26. Aliiweka ile madhabahu ya dhahabu katika hema, mbele ya pazia,

27. na kufukiza ubani wenye harufu nzuri juu yake, kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu.

28. Alitundika pazia kwenye mlango wa hema takatifu,

29. akaweka hapo langoni mwa hema takatifu madhabahu ya sadaka za kuteketezwa, akatolea juu yake sadaka ya kuteketezwa na sadaka ya nafaka, kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu.

30. Aliliweka birika la kutawadhia katikati ya hema la mkutano na madhabahu, na kutia maji ya kutawadha.

31. Mose, Aroni na wanawe, wote walinawa mikono na miguu yao humo.

32. Kila walipoingia ndani ya hema au walipokaribia ile madhabahu, walinawa, kama Mose alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu.

33. Mwishowe Mose akatengeneza ua kulizunguka hema takatifu na madhabahu, na kuweka pazia kwenye lango la ua. Hivyo, Mose akaikamilisha kazi yote.

34. Kisha, lile wingu likalifunika lile hema la mkutano, na utukufu wa Mwenyezi-Mungu ukalijaza hema.

35. Mose alishindwa kuingia ndani ya hema la mkutano kwa sababu hilo wingu lilikaa juu yake, na utukufu wa Mwenyezi-Mungu ukajaa humo.

36. Katika safari zao zote Waisraeli hawakuanza safari kamwe isipokuwa wakati wingu hilo lilipoinuliwa kutoka juu ya hema.

Kusoma sura kamili Kutoka 40