Agano la Kale

Agano Jipya

Kutoka 40:12-25 Biblia Habari Njema (BHN)

12. “Utamwita Aroni na wanawe waje mlangoni mwa hema la mkutano, kisha uwatawadhe.

13. Mvike Aroni yale mavazi matakatifu; utampaka mafuta na kumweka wakfu, ili aweze kunitumikia kama kuhani.

14. Waite wanawe na kuwavisha zile kanzu.

15. Kisha uwapake mafuta kama ulivyompaka baba yao, ili nao pia wanitumikie kama makuhani. Kupakwa mafuta huku kutawaingiza katika ukuhani wa kudumu katika vizazi vyao vyote.”

16. Basi, Mose alitekeleza kikamilifu kabisa maagizo yote ya Mwenyezi-Mungu.

17. Mnamo siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza mwaka wa pili baada ya kutoka Misri, hema la mkutano lilisimikwa.

18. Mose aliweka vikalio vyake, akainua mbao zake, akashikamanisha pau zake na kusimamisha nguzo zake.

19. Alitandaza pazia juu ya hema takatifu na kuweka kifuniko cha hema juu yake, kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu.

20. Kisha alichukua vile vibao viwili vya mawe na kuviweka katika lile sanduku. Aliipitisha ile mipiko katika vikonyo vya sanduku na kukiweka kiti cha rehema juu yake.

21. Kisha akaliweka lile sanduku la maamuzi ndani ya hema na kutundika pazia, na kwa namna hiyo akalisitiri sanduku la maamuzi, kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu.

22. Aliweka meza ndani ya hema la mkutano, upande wa kaskazini, sehemu ya nje ya pazia,

23. na juu yake akaipanga mikate iliyotolewa kwa Mwenyezi-Mungu, kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu.

24. Alikiweka kinara ndani ya hema la mkutano, upande wa kusini, mkabala wa meza.

25. Humo, mbele ya Mwenyezi-Mungu, akaziwasha taa zake, kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu.

Kusoma sura kamili Kutoka 40