Agano la Kale

Agano Jipya

Kutoka 4:18-27 Biblia Habari Njema (BHN)

18. Mose alirudi kwa Yethro, baba mkwe wake, akamwambia, “Tafadhali niruhusu nirudi Misri kwa ndugu zangu, nikaone kama bado wako hai.” Yethro akamwambia, “Nenda kwa amani.”

19. Mose akiwa bado nchini Midiani, Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Rudi Misri kwa sababu wale wote waliotaka kukuua wamekwisha kufa.”

20. Basi, Mose akamchukua mkewe na watoto wake, akawapandisha juu ya punda, akaanza safari ya kurudi Misri. Mkononi mwake alichukua ile fimbo aliyoamriwa na Mungu aichukue.

21. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Utakapofika Misri, hakikisha kwamba umetenda mbele ya Farao miujiza yote niliyokupa uwezo kuifanya. Lakini mimi nitaufanya moyo wa Farao kuwa mgumu, naye hatawaachia Waisraeli waondoke.

22. Nawe utamwambia Farao kuwa Mwenyezi-Mungu asema hivi, ‘Israeli ni mzaliwa wangu wa kwanza wa kiume!

23. Nami nakuambia: Mwache mwanangu aondoke, ili anitumikie! Kama ukikataa kumwachia aondoke, tazama nitamuua mzaliwa wako wa kwanza wa kiume.’”

24. Akiwa bado njiani kurudi Misri, Mose alikuwa mahali pa kulala wageni; basi, Mungu alikutana naye na kutaka kumuua.

25. Hapo Zipora akakimbia haraka, akachukua jiwe kali, akalikata govi la mwanawe na kumgusa nalo Mose miguuni akisema, “Wewe ni bwana harusi wa damu”.

26. Hapo Mwenyezi-Mungu akamwacha Mose. Zipora alikuwa amesema, “Bwana harusi wa damu,” kwa sababu ya kutahiri.

27. Mwenyezi-Mungu akamwambia Aroni, “Nenda jangwani ukakutane na Mose.” Basi, Aroni akaenda, akakutana na Mose kwenye mlima wa Mungu, akambusu.

Kusoma sura kamili Kutoka 4