Agano la Kale

Agano Jipya

Kutoka 35:20-35 Biblia Habari Njema (BHN)

20. Basi, jumuiya yote ya Waisraeli ikaondoka mbele ya Mose.

21. Kila mtu aliyevutwa na kusukumwa moyoni mwake alimtolea Mungu mchango wake kwa ajili ya hema la mkutano, huduma zake zote na mavazi yake matakatifu.

22. Hivyo wote wenye moyo mkarimu, wanaume kwa wanawake, wakaleta vipini, pete za mhuri, vikuku na kila aina ya vyombo vya dhahabu; kila mtu akamtolea Mwenyezi-Mungu kitu cha dhahabu.

23. Kila mtu alileta chochote alichokuwa nacho kama vile sufu ya rangi ya buluu zambarau na nyekundu, au kitani safi, au manyoya ya mbuzi au ngozi ya kondoo iliyotiwa rangi nyekundu.

24. Kila mtu aliyeweza kutoa fedha au shaba aliileta kwa Mwenyezi-Mungu kama toleo lake. Tena mtu yeyote aliyekuwa na mbao za mjohoro alileta pia.

25. Wanawake wote waliokuwa na ujuzi wa kufuma walileta vitu walivyofuma kwa sufu ya rangi ya buluu, zambarau na nyekundu na kitani safi iliyosokotwa.

26. Na wanawake wote waliokuwa na ujuzi walisokota manyoya ya mbuzi.

27. Viongozi walileta vito vya rangi na mawe mengine kwa ajili ya kizibao na kifuko cha kifuani;

28. walileta pia viungo na mafuta kwa ajili ya taa, mafuta ya kupaka na ubani wenye harufu nzuri.

29. Waisraeli wote, wanaume kwa wanawake, ambao walivutwa moyoni mwao kuleta chochote kwa ajili ya kazi ambayo Mwenyezi-Mungu alikuwa amemwagiza Mose ifanyike, walileta vitu hivyo kwa hiari, kama mchango wa kumpa Mwenyezi-Mungu.

30. Mose aliwaambia Waisraeli; “Tazameni! Mwenyezi-Mungu amemteua Bezaleli, mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa kabila la Yuda.

31. Amemjaza roho yake, amempa ujuzi, akili, maarifa na ufundi,

32. abuni michoro ya sanaa na kufanya kazi za kufua dhahabu, fedha na shaba;

33. achonge mawe ya kupambia na mbao kwa ajili ya kazi nyingine zote za kifundi.

34. Pia amemwongoza yeye na Oholiabu, mwana wa Ahisamaki, wa kabila la Dani wawafundishe wengine.

35. Amewapa ujuzi wa kufanya kila kazi ya ufundi au ifanywayo na watu wa sanaa au mafundi wa kutarizi kwa sufu ya rangi ya buluu, zambarau na nyekundu na kitani safi iliyosokotwa, kwa kutumia ufundi wowote wa msanii.

Kusoma sura kamili Kutoka 35