Agano la Kale

Agano Jipya

Kutoka 34:6-21 Biblia Habari Njema (BHN)

6. Kisha Mwenyezi-Mungu akapita mbele ya Mose akitangaza tena, “Mwenyezi-Mungu; mimi Mwenyezi-Mungu, ni Mungu mwenye huruma na neema; si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa fadhili na uaminifu.

7. Mimi nawafadhili maelfu, nikiwasamehe uovu, makosa na dhambi; lakini kwa vyovyote vile sitaacha kumwadhibu mwenye hatia; nawapatiliza watoto na wajukuu uovu wa baba na babu zao, hata kizazi cha tatu na nne.”

8. Mose akainama chini mara, akamwabudu Mungu.

9. Kisha akasema, “Ee Bwana wangu, kwa vile umenijalia fadhili mbele zako, nakuomba uende pamoja nasi. Watu hawa ni wenye vichwa vigumu, lakini utusamehe uovu wetu na dhambi yetu, utupokee kama watu wako mwenyewe.”

10. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Sasa ninafanya agano na watu wako. Nitatenda maajabu mbele yao ambayo hayajapata kutendwa duniani kote, wala katika taifa lolote. Na watu wote mnaoishi kati yao wataona matendo yangu makuu. Maana nitafanya jambo la ajabu kwa ajili yako.

11. “Shikeni amri ninazowapa leo. Nitawafukuza mbele yenu Waamori, Wakanaani, Wahiti, Waperizi, Wahivi na Wayebusi.

12. Jihadharini msije mkafanya agano na wakazi wa nchi mnayoiendea, maana hilo litakuwa mtego miongoni mwenu.

13. Lakini mtazibomoa madhabahu zao na kuzivunja nguzo zao za ibada na sanamu zao za Ashera.

14. Msiabudu mungu yeyote mwingine, maana mimi Mwenyezi-Mungu najulikana kwa jina: ‘Mwenye Wivu,’ mimi ni Mungu mwenye wivu.

15. Msifanye mikataba yoyote na wakazi wa nchi hiyo, maana watakapoiabudu miungu yao ya uongo na kuitambikia, watawaalikeni, nanyi mtashawishiwa kula vyakula wanavyoitambikia miungu yao,

16. nao wavulana wenu wakaoa binti zao, na hao binti wanaoabudu miungu yao, wakawashawishi wavulana wenu kufuata miungu yao.

17. “Msijifanyie miungu ya uongo ya chuma.

18. “Mtaiadhimisha sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu. Kwa muda wa siku saba mtakula mikate isiyotiwa chachu wakati uliopangwa katika mwezi wa Abibu, kama nilivyowaamuru, kwa sababu katika mwezi huo wa Abibu mlitoka Misri.

19. Kila mzaliwa wa kwanza wa kiume ni wangu, pamoja na wazaliwa wa kwanza wa kiume wa wanyama wako wote, wa ng'ombe na wa kondoo.

20. Mzaliwa wa kwanza wa punda utamkomboa kwa kunitolea kondoo. Kama hutamkomboa utamvunja shingo. Watoto wenu wote wa kiume ambao ni wazaliwa wa kwanza mtawakomboa. Mtu yeyote asije mbele yangu mikono mitupu.

21. “Siku sita mtafanya kazi zenu, lakini siku ya saba mtapumzika, hata ikiwa ni wakati wa kulima au kuvuna.

Kusoma sura kamili Kutoka 34