Agano la Kale

Agano Jipya

Kutoka 34:1-17 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Chonga vibao viwili vya mawe kama vile vya kwanza, nami nitayaandika maneno yale yaliyokuwa katika vile vibao vya kwanza ulivyovivunja.

2. Uwe tayari kesho asubuhi, uje kukutana nami mlimani Sinai.

3. Mtu yeyote asije pamoja nawe, wala asionekane popote mlimani; wala kondoo au ng'ombe wasilishwe karibu yake.”

4. Basi, Mose akachonga vibao viwili vya mawe kama vile vya kwanza. Akaondoka asubuhi na mapema, akapanda mlimani Sinai, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru, akiwa na vile vibao viwili vya mawe mikononi mwake.

5. Mwenyezi-Mungu akashuka katika wingu, akasimama pamoja na Mose, akalitaja jina lake, “Mwenyezi-Mungu.”

6. Kisha Mwenyezi-Mungu akapita mbele ya Mose akitangaza tena, “Mwenyezi-Mungu; mimi Mwenyezi-Mungu, ni Mungu mwenye huruma na neema; si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa fadhili na uaminifu.

7. Mimi nawafadhili maelfu, nikiwasamehe uovu, makosa na dhambi; lakini kwa vyovyote vile sitaacha kumwadhibu mwenye hatia; nawapatiliza watoto na wajukuu uovu wa baba na babu zao, hata kizazi cha tatu na nne.”

8. Mose akainama chini mara, akamwabudu Mungu.

9. Kisha akasema, “Ee Bwana wangu, kwa vile umenijalia fadhili mbele zako, nakuomba uende pamoja nasi. Watu hawa ni wenye vichwa vigumu, lakini utusamehe uovu wetu na dhambi yetu, utupokee kama watu wako mwenyewe.”

10. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Sasa ninafanya agano na watu wako. Nitatenda maajabu mbele yao ambayo hayajapata kutendwa duniani kote, wala katika taifa lolote. Na watu wote mnaoishi kati yao wataona matendo yangu makuu. Maana nitafanya jambo la ajabu kwa ajili yako.

11. “Shikeni amri ninazowapa leo. Nitawafukuza mbele yenu Waamori, Wakanaani, Wahiti, Waperizi, Wahivi na Wayebusi.

12. Jihadharini msije mkafanya agano na wakazi wa nchi mnayoiendea, maana hilo litakuwa mtego miongoni mwenu.

13. Lakini mtazibomoa madhabahu zao na kuzivunja nguzo zao za ibada na sanamu zao za Ashera.

14. Msiabudu mungu yeyote mwingine, maana mimi Mwenyezi-Mungu najulikana kwa jina: ‘Mwenye Wivu,’ mimi ni Mungu mwenye wivu.

15. Msifanye mikataba yoyote na wakazi wa nchi hiyo, maana watakapoiabudu miungu yao ya uongo na kuitambikia, watawaalikeni, nanyi mtashawishiwa kula vyakula wanavyoitambikia miungu yao,

16. nao wavulana wenu wakaoa binti zao, na hao binti wanaoabudu miungu yao, wakawashawishi wavulana wenu kufuata miungu yao.

17. “Msijifanyie miungu ya uongo ya chuma.

Kusoma sura kamili Kutoka 34