Agano la Kale

Agano Jipya

Kutoka 33:4-16 Biblia Habari Njema (BHN)

4. Watu walilia waliposikia habari hizi mbaya; wala hakuna aliyevaa mapambo yake.

5. Walifanya hivyo kwani Mwenyezi-Mungu alikuwa amemwambia Mose, “Waambie Waisraeli, ‘Nyinyi ni watu wenye vichwa vigumu; nikienda pamoja nanyi kwa muda mfupi tu, nitawaangamiza. Hivyo vueni mapambo yenu ili nijue namna ya kuwatendea.’”

6. Basi, Waisraeli waliyavua mapambo yao tangu walipoondoka mlimani Horebu.

7. Mose alikuwa na desturi ya kulichukua lile hema na kulisimika nje ya kambi. Hema hilo alilipa jina, Hema la Mkutano. Mtu yeyote aliyetaka shauri kwa Mwenyezi-Mungu alikwenda kwenye hema la mkutano nje ya kambi.

8. Kila mara Mose alipotoka kwenda kwenye hema hilo, kila mtu alisimama penye mlango wa hema lake na kumwangalia Mose mpaka alipoingia ndani ya hilo hema.

9. Wakati Mose alipoingia ndani ya hilo hema, mnara wa wingu ulitua kwenye mlango wa hema, na Mwenyezi-Mungu akaongea naye.

10. Watu wote walipouona ule mnara wa wingu umesimama mlangoni mwa hema, kila mmoja wao alisimama na kuabudu mlangoni mwa hema lake.

11. Hivyo ndivyo Mwenyezi-Mungu alivyokuwa akiongea na Mose uso kwa uso, kama mtu na rafiki yake. Kisha Mose alirudi tena kambini. Naye kijana Yoshua mwana wa Nuni ambaye alikuwa mtumishi wake hakuondoka hemani.

12. Mose akamwambia Mwenyezi-Mungu, “Tazama! Wewe waniambia, ‘Waongoze watu hawa,’ lakini hujanijulisha ni nani utakayemtuma anisaidie. Hata hivyo umesema kwamba unanijua kwa jina na pia kwamba nimepata fadhili mbele zako.

13. Sasa basi, nakusihi, kama kweli nimepata fadhili mbele yako, nioneshe sasa njia zako, ili nipate kukujua na kupata fadhili mbele zako. Naomba ukumbuke pia kwamba taifa hili ni watu wako.”

14. Mungu akasema, “Mimi mwenyewe nitakwenda pamoja nawe, na nitakupa faraja.”

15. Mose akasema, “Kama wewe binafsi hutakwenda pamoja nami, basi, usituondoe mahali hapa.

16. Maana nitajuaje kuwa nimepata fadhili mbele zako, mimi na watu wako kama usipokwenda pamoja nasi? Ukienda pamoja nasi itatufanya mimi na watu wako kuwa watu wa pekee miongoni mwa watu wote duniani.”

Kusoma sura kamili Kutoka 33