Agano la Kale

Agano Jipya

Kutoka 32:16-28 Biblia Habari Njema (BHN)

16. Vibao hivyo vilikuwa kazi yake Mungu mwenyewe na maandishi hayo aliyachora Mungu mwenyewe.

17. Yoshua aliposikia kelele za watu, akamwambia Mose, “Kuna kelele za vita kambini.”

18. Lakini Mose akamjibu, “Si kelele ya ushindi au kushindwa, bali kelele ninayosikia ni kelele ya watu wanaoimba.”

19. Mara tu walipoikaribia kambi walipomwona yule ndama na watu wakicheza; hapo hasira ya Mose ikawaka kama moto, akavitupa chini vile vibao kutoka mikononi mwake na kuvivunja pale chini ya mlima.

20. Basi, akamchukua yule ndama akamchoma moto, akamsaga mpaka akawa unga, akaukoroga unga huo katika maji na kuwalazimisha Waisraeli wanywe.

21. Mose akamwuliza Aroni, “Walikufanya nini watu hawa hata ukawaingiza katika dhambi kubwa hivyo?”

22. Aroni akamjibu, “Nakuomba ee bwana wangu hasira yako isiniwakie mimi mtumishi wako. Unawafahamu jinsi watu hawa walivyo tayari kutenda maovu.

23. Walikuja wakaniambia, ‘Tufanyie miungu ambayo itatuongoza kwani huyo Mose aliyetutoa nchini Misri hatujui lililompata’.

24. Nami nikawaambia, kila mmoja aliye na vito vya dhahabu na avilete. Basi, wakaniletea, nami nikaviyeyusha motoni na huyu ndama akatokea.”

25. Basi, Mose alipoona kuwa watu wameasi na kufanya wapendavyo (kwa kuwa Aroni aliwafanya waasi na kufanya wapendavyo, na kujiletea aibu mbele ya adui zao),

26. Mose akasimama mbele ya lango la kambi na kuuliza, “Ni nani aliye upande wa Mwenyezi-Mungu? Na aje kwangu.” Wana wote wa Lawi wakakusanyika pamoja mbele yake.

27. Akawaambia, “Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, anasema hivi: ‘Kila mtu na ajifunge upanga wake kiunoni, azunguke kila mahali kambini, kutoka lango moja hadi lingine, na kila mmoja amuue ndugu yake, rafiki yake na jirani yake.’”

28. Wana wa Lawi wakafanya kama Mose alivyowaagiza. Siku hiyo waliuawa watu wapatao 3,000.

Kusoma sura kamili Kutoka 32