Agano la Kale

Agano Jipya

Kutoka 3:13-18 Biblia Habari Njema (BHN)

13. Hapo, Mose akamwambia Mungu, “Sasa, nikiwaendea Waisraeli na kuwaambia, ‘Mungu wa babu zenu amenituma kwenu,’ nao wakiniuliza, ‘Jina lake ni nani,’ nitawaambia nini?”

14. Mungu akamjibu, “MIMI NDIMI NILIYE. Waambie hivi watu wa Israeli: Yule anayeitwa, NDIMI NILIYE, amenituma kwenu.

15. Waambie hivi Waisraeli: Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zenu, Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka, Mungu wa Yakobo, amenituma kwenu. Hili ndilo jina langu milele, na hivyo ndivyo nitakavyokumbukwa katika vizazi vyote.

16. Nenda ukawakusanye wazee wa Israeli na kuwaambia: Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zenu: Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka, Mungu wa Yakobo, amenitokea na kusema, ‘Nimewachunguzeni na kuyaona mambo mnayotendewa nchini Misri!

17. Naahidi kuwa nitawatoa katika mateso yenu huko Misri na kuwapeleka katika nchi ya Wakanaani, Wahiti, Waamori, Waperizi, Wahivi na Wayebusi; nitawapeleka katika nchi inayotiririka maziwa na asali.’

18. “Wao watakusikiliza, nawe pamoja na wazee wa Waisraeli mtamwendea mfalme wa Misri na kumwambia, ‘Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Waebrania, ametutokea. Sasa, uturuhusu tuende safari ya mwendo wa siku tatu jangwani, tukamtambikie Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu.’

Kusoma sura kamili Kutoka 3