Agano la Kale

Agano Jipya

Kutoka 29:30-46 Biblia Habari Njema (BHN)

30. Mwana wa Aroni atakayekuwa kuhani mahali pa baba yake atayavaa mavazi hayo siku saba katika hema la mkutano, ili kuhudumu katika mahali patakatifu.

31. “Utachukua nyama ya huyo kondoo wa kuwaweka wakfu na kuichemshia katika mahali patakatifu.

32. Kisha utawapa Aroni na wanawe, nao wataila mlangoni pa hema la mkutano pamoja na ile mikate iliyosalia kapuni.

33. Watavila vitu hivyo vilivyotumika kuwaweka wakfu na kwa ajili ya kuwafanyia upatanisho, lakini mtu mwingine asiruhusiwe kuvila kwani ni vitakatifu.

34. Kama nyama yoyote au mikate hiyo itasalia mpaka asubuhi yake, basi utaiteketeza kwa moto; isiliwe maana ni kitu kitakatifu.

35. “Hivyo ndivyo utakavyowatendea Aroni na wanawe kufuatana na yote yale niliyokuamuru; utawaweka wakfu kwa muda wa siku saba,

36. na kila siku utatoa fahali awe sadaka ya kuondolea dhambi ili kufanya upatanisho, na kwa kufanya hivyo utaitakasa madhabahu; kisha utaimiminia mafuta ili kuiweka wakfu.

37. Kwa siku saba utaifanyia madhabahu upatanisho na kuiweka wakfu. Baada ya hayo, madhabahu itakuwa takatifu kabisa na chochote kitakachoigusa kitakuwa kitakatifu.

38. “Kila siku, wakati wote ujao, utatolea sadaka juu ya madhabahu: Wanakondoo wawili wenye umri wa mwaka mmoja.

39. Mwanakondoo mmoja utamtoa sadaka asubuhi na mwingine jioni.

40. Pamoja na mwanakondoo wa kwanza, utatoa kilo moja ya unga laini uliochanganywa na lita moja ya mafuta safi, na lita moja ya divai kama sadaka ya kinywaji.

41. Hali kadhalika na yule mwanakondoo mwingine wa jioni utamtolea tambiko pamoja na sadaka ya nafaka na ya kinywaji kama ulivyofanya asubuhi; harufu ya tambiko hiyo inayotolewa kwa moto itanipendeza mimi Mwenyezi-Mungu.

42. Sadaka hii ya kuteketezwa itatolewa daima, kizazi hata kizazi, mbele yangu mimi Mwenyezi-Mungu, mbele ya mlango wa hema la mkutano ambapo mimi nitakutana nanyi na kuongea nanyi.

43. Hapo ndipo nitakapokutana na Waisraeli na utukufu wangu utapafanya pawe patakatifu.

44. Hema la mkutano na madhabahu nitavifanya vitakatifu; vilevile Aroni na wanawe nitawaweka wakfu ili wanitumikie kama makuhani.

45. Nitaishi kati ya Waisraeli, nami nitakuwa Mungu wao.

46. Hapo ndipo watakapotambua kuwa mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, niliyewaleta kutoka nchi ya Misri, ili niishi kati yao. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wao.

Kusoma sura kamili Kutoka 29