Agano la Kale

Agano Jipya

Kutoka 29:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)

1. “Haya ndiyo mambo utakayowafanyia Aroni na wanawe ili kuwaweka wakfu wanitumikie kama makuhani. Utachukua ndama dume na kondoo madume wawili wasio na dosari,

2. mikate isiyotiwa chachu, maandazi yasiyotiwa chachu yaliyokandwa kwa mafuta, na mikate myembamba isiyotiwa chachu, lakini iliyopakwa mafuta. Vyote hivi viwe vimetengenezwa kwa unga laini wa ngano.

3. Kisha iweke hiyo mikate ndani ya kikapu kimoja na kunitolea wakati mmoja na yule ndama dume na wale kondoo dume wawili.

4. “Kisha wapeleke Aroni na wanawe mlangoni pa hema la mkutano na kuwatawadha.

5. Kisha utachukua yale mavazi ya kikuhani umvike Aroni: Joho, kanzu, kizibao, kifuko cha kifuani, na kumfunga ule mshipi uliofumwa kwa ustadi.

6. Tena utamvika kile kilemba kichwani na kuweka juu ya hicho kilemba ile taji takatifu.

7. Baada ya kufanya hivyo, utachukua yale mafuta ya kupaka, ummiminie Aroni kichwani mwake kumweka wakfu.

8. “Kisha utawaleta wana wa Aroni na kuwavika vizibao.

9. Utawafunga mishipi viunoni na kuwavisha kofia zao. Hivyo ndivyo utakavyowaweka wakfu Aroni na wanawe kuwa makuhani. Hao watakuwa makuhani daima.

10. “Kisha utamleta yule ndama dume mbele ya hema la mkutano. Aroni na wanawe wataweka mikono yao juu ya kichwa cha ndama huyo

11. na kumchinja mbele ya Mwenyezi-Mungu, mlangoni pa hema la mkutano.

12. Utachukua kiasi cha damu na kuipaka kwenye pembe za madhabahu kwa kidole chako, na damu yote inayosalia utaimwaga chini ya madhabahu.

Kusoma sura kamili Kutoka 29