Agano la Kale

Agano Jipya

Kutoka 28:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)

1. “Nawe Mose umlete kwangu Aroni ndugu yako, pamoja na wanawe: Nadabu, Abihu, Eleazari na Ithamari utawateua miongoni mwa Waisraeli, ili wanitumikie kama makuhani.

2. Utamshonea ndugu yako Aroni mavazi matakatifu ili apate kuonekana mwenye utukufu na mzuri.

3. Waagize mafundi wote ambao nimewapa maarifa wamtengenezee Aroni mavazi ili awekwe wakfu kwa ajili ya kazi ya ukuhani.

4. Waambie wamtengenezee vitu vifuatavyo: Kifuko cha kifuani, kizibao, kanzu, joho iliyonakshiwa, kilemba na mshipi. Aroni nduguyo na wanawe watayavaa ili wanitumikie kama makuhani.

5. Hao mafundi watatumia sufu ya rangi ya buluu, zambarau na nyekundu, na nyuzi za dhahabu na kitani safi iliyosokotwa.

6. “Watakitengeneza kizibao cha kuhani kwa nyuzi za dhahabu na sufu ya rangi ya buluu, zambarau na nyekundu, na kitani safi iliyosokotwa, na kukitarizi vizuri.

7. Kitakuwa na kamba mbili za kukifungia mabegani zilizoshonewa kwenye ncha zake mbili.

8. Mkanda wa kukishikia utatengenezwa kwa vifaa hivyohivyo: Kwa nyuzi za dhahabu, sufu ya buluu, zambarau na nyekundu, na kitani safi iliyosokotwa na kuwa kitu kimoja na kizibao hicho.

9. “Kisha utachukua mawe mawili ya sardoniki ambayo utachora juu yake majina ya wana wa Israeli.

10. Majina sita katika jiwe la kwanza, na majina sita yaliyobakia katika jiwe la pili; majina yafuatane kadiri ya kuzaliwa kwao.

11. Utayachora majina hayo juu ya hayo mawe kama vile sonara achoravyo mhuri, kisha uyatie nakshi na kuyaingiza katika vijalizo vya dhahabu.

Kusoma sura kamili Kutoka 28