Agano la Kale

Agano Jipya

Kutoka 24:8-18 Biblia Habari Njema (BHN)

8. Mose akaichukua ile damu na kuwanyunyizia watu, akisema, “Hii ndiyo damu ya agano ambalo Mwenyezi-Mungu amelifanya nanyi kufuatana na maneno haya yote.”

9. Kisha Mose, Aroni, Nadabu na Abihu na wazee sabini wa Israeli wakapanda mlimani,

10. wakamwona Mungu wa Israeli. Chini ya miguu yake kulikuwa na kitu kama sakafu ya mawe ya johari ya rangi ya samawati, kikiwa safi kama mbingu angavu.

11. Na Mungu hakuwadhuru hao viongozi wa watu wa Israeli. Walimwona Mungu, wakala na kunywa.

12. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Njoo kwangu juu mlimani, ungoje huko. Mimi nitakupa vibao viwili vya mawe vyenye sheria na amri nilizoandika kwa ajili ya kuwafunza Waisraeli.”

13. Basi, Mose akaondoka pamoja na Yoshua, mtumishi wake, akaenda kwenye mlima wa Mungu.

14. Mose aliwaambia wale wazee, “Tungojeni hapa mpaka tutakapowarudia. Aroni na Huri wako pamoja nanyi; yeyote aliye na tatizo na awaendee wao.”

15. Basi, Mose akaenda mlimani, na wingu likaufunika mlima.

16. Utukufu wa Mwenyezi-Mungu ukatua juu ya mlima Sinai na wingu likaufunika mlima kwa muda wa siku sita. Siku ya saba Mungu akamwita Mose kutoka katikati ya lile wingu.

17. Utukufu wa Mwenyezi-Mungu ulionekana mbele ya macho ya watu wa Israeli kama moto unaowaka juu ya mlima.

18. Mose akaingia ndani ya lile wingu, akapanda mlimani. Alikaa huko kwa muda wa siku arubaini, mchana na usiku.

Kusoma sura kamili Kutoka 24