Agano la Kale

Agano Jipya

Kutoka 21:15-27 Biblia Habari Njema (BHN)

15. “Ampigaye baba yake au mama yake lazima auawe.

16. “Amtekaye mtu nyara ili kumwuza au kumfanya mtumwa wake lazima auawe.

17. “Amlaaniye baba yake au mama yake lazima auawe.

18. “Watu wawili wakigombana, kisha mmoja akampiga mwenzake jiwe au ngumi bila kumwua, lakini akamjeruhi kiasi cha kumfanya augue na kulala kitandani,

19. iwapo huyo aliyepigwa atapata nafuu na kuweza kutembea kwa kutegemea fimbo, huyo aliyemjeruhi atasamehewa. Lakini, atamlipa fidia ya muda alioupoteza kitandani, na kuhakikisha amemwuguza mpaka apone kabisa.

20. “Mtu akimpiga mtumwa wake wa kiume au wa kike kwa fimbo na kumwua papo hapo, ni lazima aadhibiwe.

21. Lakini mtumwa huyo akibaki hai siku moja au mbili, bwana wake hataadhibiwa, kwani huyo alikuwa ni mali yake.

22. “Wanaume wakipigana na kumwumiza mwanamke mjamzito, hata mimba yake ikaharibika bila madhara mengine zaidi, yule aliyemwumiza atatozwa faini kama atakavyodai mumewe mwanamke huyo na kama mahakimu watakavyoamua.

23. Lakini kama yatakuwapo madhara mengine, basi, lazima amlipe uhai kwa uhai,

24. jicho kwa jicho, jino kwa jino, mkono kwa mkono, mguu kwa mguu,

25. kuchomwa moto kwa kuchomwa moto, jeraha kwa jeraha, na pigo kwa pigo.

26. “Mtu akimpiga jicho mtumwa wake wa kiume au wa kike na kuliharibu jicho lake, ni lazima amwachilie aende huru bila malipo kwa ajili ya jicho lake.

27. Hali kadhalika, akimpiga hata kumngoa jino mtumwa wake wa kiume au wa kike, ni lazima amwachilie huru kwa ajili ya jino lake.

Kusoma sura kamili Kutoka 21