Agano la Kale

Agano Jipya

Kutoka 21:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)

1. “Haya ndiyo maagizo utakayowapa Waisraeli:

2. Ukimnunua mtumwa Mwebrania, atakutumikia kwa miaka sita, lakini mwaka wa saba atakuwa huru na kuondoka, bila malipo.

3. Kama alinunuliwa kabla hajaoa, ataondoka peke yake. Lakini kama alikuja na mkewe, basi, ataondoka na mkewe.

4. Kama bwana wake alimwoza mke, akamzalia watoto wa kike au wa kiume, basi, huyo mwanamke na watoto wake watakuwa mali ya huyo bwana wake, na huyo mtumwa ataondoka peke yake.

5. Lakini kama mtumwa huyo akisema kwamba anampenda bwana wake, mke wake na watoto wake na hataki kuondoka na kuwa huru,

6. basi, bwana wake atamleta mbele ya Mungu. Kisha atampeleka kwenye mlango au kizingitini na kumtoboa sikio lake kwa shazia; naye atamtumikia bwana wake maisha yake yote.

7. “Mtu akimwuza binti yake kuwa mtumwa, huyo hatapata uhuru wake kama watumwa wa kiume.

8. Ikiwa huyo bwana wake alimnunua awe mmoja wa wake zake, kisha asipendezwe naye, huyo bwana atamwacha baba yake huyo mtumwa amkomboe. Huyo bwana hana haki ya kumwuza kwa watu wa mataifa mengine, kwa kuwa atakuwa amekosa uaminifu.

9. Kama ataamua kumwoza kwa mwanawe, atamtendea mtumwa huyo kama binti yake.

10. Kama huyo bwana akioa mke mwingine, lazima aendelee kumtosheleza mkewe wa kwanza kwa chakula, mavazi na haki zake za ndoa.

11. Iwapo huyo bwana hatamtimizia haki hizo tatu, basi, mke ataondoka na kuwa huru bila malipo yoyote.

Kusoma sura kamili Kutoka 21