Agano la Kale

Agano Jipya

Kutoka 20:8-22 Biblia Habari Njema (BHN)

8. “Usisahau kuiweka takatifu siku ya Sabato.

9. Siku sita fanya kazi na tenda mambo yako yote.

10. Lakini siku ya saba ni Sabato ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wako. Siku hiyo usifanye kazi yoyote, wewe, wala mwanao, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala watumishi wako wa kike, wala mnyama wako wa kufugwa, wala mgeni aliye nyumbani mwako.

11. Maana kwa siku sita mimi Mwenyezi-Mungu niliziumba mbingu na dunia, bahari na vyote vilivyomo, kisha nikapumzika siku ya saba. Kwa hiyo mimi Mwenyezi-Mungu niliibariki siku ya Sabato, nikaitakasa.

12. “Waheshimu baba yako na mama yako, ili uishi maisha marefu katika nchi ninayokupa mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako.

13. “Usiue.

14. “Usizini.

15. “Usiibe.

16. “Usimshuhudie jirani yako uongo.

17. “Usiitamani nyumba ya jirani yako, wala mke wake, wala mtumwa wake wa kiume au wa kike, wala ng'ombe wake, wala punda wake, wala chochote kilicho mali ya jirani yako.”

18. Watu waliposikia ngurumo na kuona umeme ukiwaka na kuisikia sauti ya parapanda juu ya mlima uliokuwa unafuka moshi, wote waliogopa na kutetemeka. Wote walisimama mbali,

19. wakamwambia Mose, “Ongea nasi wewe mwenyewe, nasi tutakusikiliza, lakini Mwenyezi-Mungu asiongee nasi, tusije tukafa.”

20. Mose akawaambia, “Msiogope, maana Mungu amekuja kuwajaribu ili mpate kumcha yeye daima na msitende dhambi.”

21. Watu wote walisimama mbali wakati Mose alipokaribia lile wingu zito alimokuwamo Mungu.

22. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Waambie Waisraeli: ‘Mmejionea nyinyi wenyewe kwamba nimeongea nanyi kutoka mbinguni.

Kusoma sura kamili Kutoka 20