Agano la Kale

Agano Jipya

Kutoka 2:9-15 Biblia Habari Njema (BHN)

9. Binti Farao akamwambia huyo mama, “Mtunze mtoto huyu, umlee kwa niaba yangu, nami nitakulipa mshahara wako.” Basi, huyo mama akamchukua mtoto, akamlea.

10. Mtoto alipokuwa mkubwa kiasi, mama yake akampeleka kwa binti Farao, naye akamchukua na kumfanya mwanawe. Binti Farao akasema, “Nimemtoa majini,” kwa hiyo akampa mtoto huyo jina Mose.

11. Siku moja, Mose alipokuwa mtu mzima, aliwaendea Waebrania wenzake ili kujionea taabu zao. Basi, akamwona Mmisri mmoja anampiga Mwebrania, mmoja wa ndugu zake Mose.

12. Mose akatazama huku na huko, na alipoona kwamba hakuna mtu karibu, alimuua yule Mmisri na kumficha mchangani.

13. Kesho yake, Mose alitoka tena, akaona Waebrania wawili wanapigana. Basi, akamwuliza yule aliyekosea, “Kwa nini unampiga mwenzako?”

14. Naye akamjibu, “Nani aliyekuweka wewe kuwa mkuu na mwamuzi wetu? Je, unataka kuniua kama ulivyomuua yule Mmisri?” Hivyo, Mose aliogopa na kufikiri, “Bila shaka jambo hilo limejulikana!”

15. Naye Farao aliposikia juu ya tukio hilo akakusudia kumuua Mose. Lakini Mose alimkimbia Farao, akaenda kukaa katika nchi ya Midiani.Siku moja, Mose alikuwa ameketi kando ya kisima cha maji.

Kusoma sura kamili Kutoka 2