Agano la Kale

Agano Jipya

Kutoka 2:12-25 Biblia Habari Njema (BHN)

12. Mose akatazama huku na huko, na alipoona kwamba hakuna mtu karibu, alimuua yule Mmisri na kumficha mchangani.

13. Kesho yake, Mose alitoka tena, akaona Waebrania wawili wanapigana. Basi, akamwuliza yule aliyekosea, “Kwa nini unampiga mwenzako?”

14. Naye akamjibu, “Nani aliyekuweka wewe kuwa mkuu na mwamuzi wetu? Je, unataka kuniua kama ulivyomuua yule Mmisri?” Hivyo, Mose aliogopa na kufikiri, “Bila shaka jambo hilo limejulikana!”

15. Naye Farao aliposikia juu ya tukio hilo akakusudia kumuua Mose. Lakini Mose alimkimbia Farao, akaenda kukaa katika nchi ya Midiani.Siku moja, Mose alikuwa ameketi kando ya kisima cha maji.

16. Basi, binti saba wa kuhani mmoja wa huko Midiani walifika kuchota maji na kuwanywesha kondoo na mbuzi wa baba yao.

17. Wachungaji wengine wakaja na kuwafukuza hao binti. Lakini Mose akawasaidia binti hao na kuwanywesha wanyama wao.

18. Walipomrudia baba yao Reueli, yeye akawauliza, “Mbona leo mmerudi upesi hivyo?”

19. Nao wakamjibu, “Mmisri mmoja alituokoa mikononi mwa wale wachungaji, naye mwenyewe akachota maji na kuwanywesha wanyama wetu.”

20. Baba yao akawauliza binti zake, “Yuko wapi? Mbona mmemwacha huko? Mwiteni aje ale chakula.”

21. Mose akakubali kukaa kwa huyo mtu. Basi, huyo mtu akampa Mose binti yake aitwaye Zipora awe mke wake.

22. Zipora akamzalia mtoto wa kiume. Mose akasema, “Nimekimbilia katika nchi ya kigeni”, kwa hiyo akampa huyo mtoto jina Gershomu.

23. Baada ya muda mrefu, mfalme wa Misri akafa. Waisraeli wakapiga kite na kulia kutokana na hali yao ya utumwa, na kilio chao kikamfikia Mungu juu.

24. Mungu akasikia kilio chao, naye akakumbuka agano alilofanya na Abrahamu, na Isaka na Yakobo.

25. Mungu aliwaangalia Waisraeli, akaona kuwa hali yao ni mbaya.

Kusoma sura kamili Kutoka 2