Agano la Kale

Agano Jipya

Kutoka 2:1-13 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Kulikuwa na mtu mmoja wa ukoo wa Walawi aliyemwoa mwanamke mmoja ambaye pia alikuwa wa ukoo wa Walawi.

2. Basi, mama huyu akapata mimba, akajifungua mtoto wa kiume. Alipoona kwamba mtoto huyo mchanga alikuwa mzuri, akamficha kwa muda wa miezi mitatu.

3. Lakini kwa vile hakuweza kumficha zaidi ya muda huo, alitengeneza namna ya kikapu cha mafunjo, akakipaka namna ya lami, akamtia huyo mtoto ndani. Kisha akakiweka kikapu kando ya mto Nili kwenye majani.

4. Dada yake huyo mtoto akajificha karibu na mahali hapo ili aone yatakayompata nduguye.

5. Basi, binti Farao akashuka mtoni kuoga, na watumishi wake wakawa wanatembeatembea kandokando ya mto. Binti Farao akakiona kile kikapu katika majani, akamtuma mjakazi wake akichukue.

6. Alipokifungua, alimwona yule mtoto mchanga, analia. Basi, akamwonea huruma, akasema, “Huyu ni mmojawapo wa watoto wa Waebrania.”

7. Papo hapo dada yake yule mtoto akajitokeza, akamwambia binti Farao, “Je, niende nikakutafutie yaya miongoni mwa wanawake wa Kiebrania akulelee mtoto huyu?”

8. Binti Farao akamwambia, “Naam; nenda.” Basi, huyo msichana akaenda, akamwita mama yake huyo mtoto.

9. Binti Farao akamwambia huyo mama, “Mtunze mtoto huyu, umlee kwa niaba yangu, nami nitakulipa mshahara wako.” Basi, huyo mama akamchukua mtoto, akamlea.

10. Mtoto alipokuwa mkubwa kiasi, mama yake akampeleka kwa binti Farao, naye akamchukua na kumfanya mwanawe. Binti Farao akasema, “Nimemtoa majini,” kwa hiyo akampa mtoto huyo jina Mose.

11. Siku moja, Mose alipokuwa mtu mzima, aliwaendea Waebrania wenzake ili kujionea taabu zao. Basi, akamwona Mmisri mmoja anampiga Mwebrania, mmoja wa ndugu zake Mose.

12. Mose akatazama huku na huko, na alipoona kwamba hakuna mtu karibu, alimuua yule Mmisri na kumficha mchangani.

13. Kesho yake, Mose alitoka tena, akaona Waebrania wawili wanapigana. Basi, akamwuliza yule aliyekosea, “Kwa nini unampiga mwenzako?”

Kusoma sura kamili Kutoka 2