Agano la Kale

Agano Jipya

Kutoka 19:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Siku ya kwanza ya mwezi wa tatu tangu walipotoka nchini Misri, watu wa Israeli walifika katika jangwa la Sinai.

2. Walipoondoka Refidimu na kufika jangwa la Sinai, huko walipiga kambi mbele ya mlima Sinai.

3. Basi, Mose akapanda juu mlimani kwa Mungu. Hapo Mwenyezi-Mungu akamwita Mose kutoka huko juu mlimani, akamwambia, “Hivi ndivyo utakavyowaambia wazawa wa Yakobo, hao Waisraeli,

4. ‘Nyinyi wenyewe mmeona nilivyowatenda Wamisri na jinsi nilivyowachukua kama tai anavyochukua watoto wake kwa mabawa, nikawaleta kwangu.

5. Sasa basi, kama mkiitii sauti yangu na kulishika agano langu, mtakuwa watu wangu wateule kati ya mataifa yote, maana dunia yote ni yangu.

6. Mtakuwa kwangu ufalme wa makuhani na taifa takatifu.’ Hayo ndiyo maneno utakayowaambia Waisraeli.”

7. Basi, Mose akarudi, akawakusanya pamoja wazee wa Waisraeli na kuwaambia maneno hayo aliyoamriwa na Mwenyezi-Mungu.

8. Watu wote wakaitikia kwa pamoja wakisema, “Mambo yote aliyoyasema Mwenyezi-Mungu, tutayafanya.” Mose akamjulisha Mwenyezi-Mungu jibu hilo la watu.

9. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Haya, mimi nitakujia katika wingu zito ili Waisraeli wapate kunisikia ninaposema nawe na kukuamini siku zote.”Kisha Mose akamwambia Mungu jinsi watu walivyosema.

10. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Nenda kwa watu uwatakase leo na kesho. Waambie wayafue mavazi yao

11. wawe tayari kwa kesho kutwa, maana siku hiyo ya tatu mimi Mwenyezi-Mungu nitashuka juu ya mlima Sinai mbele ya watu wote.

12. Tena wewe utawawekea watu mpaka kuzunguka mlima. Utawakanya wajihadhari sana wasipande juu mlimani wala kuugusa mpaka wake. Yeyote atakayeugusa mlima, atauawa.

Kusoma sura kamili Kutoka 19