Agano la Kale

Agano Jipya

Kutoka 16:12-26 Biblia Habari Njema (BHN)

12. “Nimeyasikia manunguniko ya Waisraeli. Basi, waambie kwamba wakati wa jioni watakula nyama, na asubuhi watakula mkate. Hapo ndipo mtakapotambua kuwa mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.”

13. Basi, mnamo wakati wa jioni kukaja kware wengi, wakafunika kambi ya Waisraeli. Asubuhi yake kukatokea umande, ukatanda kandokando ya kambi yao.

14. Umande huo ulipotoweka, kukabaki huko nyikani kitu kama mkate mwembamba na mwepesi.

15. Waisraeli walipoona kitu hicho walishangaa, wakaulizana, “Nini hiki?” Hawakujua kilikuwa kitu gani. Basi, Mose akawaambia, “Huu ni mkate ambao Mwenyezi-Mungu amewapa mle.

16. Mwenyezi-Mungu ameamuru mfanye hivi: Kila mtu na akusanye chakula kiasi anachoweza kula; ataokota kiasi cha pishi moja kwa kila mtu hemani mwake.”

17. Basi, Waisraeli wakafanya hivyo, na ikawa kwamba, wengine waliokota kwa wingi na wengine kidogo.

18. Lakini wote walipokipima kipimo walichookota katika pishi, waligundua kuwa aliyeokota kingi hakuwa na cha ziada, na aliyeokota kidogo, hakupungukiwa. Kila mmoja alikuwa ameokota kiasi alichoweza kula.

19. Mose akawaambia watu, “Mtu yeyote asibakize chakula hicho mpaka asubuhi.”

20. Lakini watu hawakumsikiliza Mose. Baadhi yao walijibakizia chakula mpaka asubuhi. Lakini asubuhi chakula hicho kikawa kimeoza na kuwa na mabuu. Mose akawakasirikia sana watu.

21. Basi, kila asubuhi walikusanya chakula kila mtu kiasi alichohitaji kula. Jua lilipopanda juu na kuwa kali, kile chakula kingine kiliyeyuka.

22. Katika siku ya sita, Waisraeli walikusanya chakula hicho maradufu, pishi nne kwa kila mtu. Basi, wazee wote wa jumuiya ya Waisraeli walimwendea Mose, wakamweleza jambo hilo.

23. Mose akawaambia, “Hii ndiyo amri ya Mwenyezi-Mungu. Kesho ni siku rasmi ya mapumziko; ni Sabato takatifu ya Mwenyezi-Mungu. Basi, nendeni mkapike au mkachemshe kile chakula mnachohitaji leo, na chakula kitakachosalia kiwekeni mpaka kesho.”

24. Basi, wakafanya hivyo na kukiacha chakula kingine mpaka kesho yake kama Mose alivyosema. Asubuhi yake waliona kwamba hakikuharibika wala kuwa na mabuu.

25. Basi, Mose akawaambia, “Kuleni chakula hicho kilichosalia kwa sababu leo ni Sabato ya Mwenyezi-Mungu. Leo hamtapata chakula huko nje.

26. Kwa siku sita mtakuwa mkikusanya chakula hiki, lakini siku ya saba ambayo ni Sabato hakitakuwapo.”

Kusoma sura kamili Kutoka 16