Agano la Kale

Agano Jipya

Kutoka 14:2-14 Biblia Habari Njema (BHN)

2. “Waambie Waisraeli warudi nyuma, wapige kambi mbele ya Pi-hahirothi, kati ya mji wa Migdoli na bahari ya Shamu, mbele ya Baal-sefoni. Mtapiga kambi mbele yake karibu na bahari.

3. Maana, Farao atafikiri, ‘Hao Waisraeli wanatangatanga, nalo jangwa limewazuia wasiweze kutoka.’

4. Hapo mimi nitamfanya Farao kuwa mkaidi, naye atawafuatia. Nami nitajipatia utukufu kwa kumwangamiza yeye na jeshi lake. Hapo Wamisri watatambua kwamba mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.” Basi, Waisraeli wakafanya hivyo.

5. Farao, mfalme wa Misri, aliposikia kwamba Waisraeli wamekimbia, yeye na maofisa wake walibadili fikira zao, wakasema, “Tumefanya nini kuwaachia Waisraeli waende zao wasitutumikie tena?”

6. Basi, Farao akatayarisha gari lake la vita na jeshi lake.

7. Alichukua magari yake bora ya vita 600 na magari yote mengine ya kivita ya Misri yakiongozwa na maofisa wa kijeshi.

8. Mwenyezi-Mungu akamfanya Farao, mfalme wa Misri, kuwa mkaidi naye akawafuatia Waisraeli ambao walikuwa wameondoka Misri kwa ushupavu.

9. Wamisri pamoja na farasi wao wote, magari ya farasi ya vita na wapandafarasi wake waliwafuata Waisraeli, wakawakuta wamepiga kambi kando ya bahari, karibu na Pi-hahirothi, mbele ya Baal-sefoni.

10. Waisraeli walipotazama na kumwona Farao akija na jeshi lake dhidi yao, walishikwa na hofu kubwa, wakamlilia Mwenyezi-Mungu.

11. Wakamwambia Mose, “Je, hapakuwa na makaburi ya kutosha nchini Misri hata ukatuleta tufie huku jangwani? Mbona umetutendea haya, kwa tututoa katika nchi ya Misri?

12. Je, hatukukuambia mambo haya tulipokuwa bado Misri? Tulikuambia utuache tuendelee kuwatumikia Wamisri. Ingalikuwa afadhali kuwatumikia Wamisri kuliko kufia huku jangwani.”

13. Mose akawaambia Waisraeli, “Msiogope! Kaeni imara! Leo mtaona jinsi Mwenyezi-Mungu atakavyowaokoa. Maana, hawa Wamisri mnaowaona leo, hamtawaona tena.

14. Mwenyezi-Mungu atawapigania; nyinyi mnachotakiwa kufanya ni kutulia tu.”

Kusoma sura kamili Kutoka 14