Agano la Kale

Agano Jipya

Kutoka 12:11-17 Biblia Habari Njema (BHN)

11. Na hivi ndivyo mtakavyomla mnyama huyo: Mtakuwa mmejifunga mikanda viunoni mwenu, mmevaa viatu na fimbo zenu mikononi. Tena mtamla kwa haraka. Hiyo ni Pasaka ya Mwenyezi-Mungu.

12. “Usiku huo, nitapita katika nchi ya Misri na kuwaua wazaliwa wa kwanza wa Misri, watu kwa wanyama. Nitaiadhibu miungu yote ya Misri. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.

13. Basi, ile damu itakuwa ishara yenu ya kuonesha nyumba mtakamokuwa. Nami nitakapoiona hiyo damu, nitawapita nyinyi, na hamtapatwa na dhara lolote wakati nitakapoipiga nchi ya Misri.

14. Vizazi hata vizazi mtaadhimisha tukio hilo kwa sikukuu kubwa kwa heshima yangu mimi Mwenyezi-Mungu. Hilo litakuwa agizo la milele kwenu.”

15. Mwenyezi-Mungu akasema, “Kwa muda wa siku saba, mtakula mikate isiyotiwa chachu. Siku ya kwanza ya siku hizo saba, mtaondoa chachu katika nyumba zenu. Mtu yeyote akila kitu kilichotiwa chachu katika muda huo wa siku saba, ni lazima aondolewe miongoni mwa Waisraeli.

16. Siku ya kwanza na siku ya saba mtakuwa na mkutano mtakatifu. Katika siku hizo mbili hamtaruhusiwa kufanya kazi yoyote isipokuwa kazi ya lazima ya kutayarisha chakula.

17. Mtaadhimisha sikukuu hii ya mikate isiyotiwa chachu kama ukumbusho wa siku nilipowatoa nyinyi, vikundi vya Israeli, kutoka Misri. Sikukuu hiyo itaadhimishwa na vizazi vyenu vyote vijavyo, kama agizo la milele.

Kusoma sura kamili Kutoka 12