Agano la Kale

Agano Jipya

Kutoka 10:13-29 Biblia Habari Njema (BHN)

13. Basi, Mose akainyosha fimbo yake juu ya nchi ya Misri. Mwenyezi-Mungu akaleta upepo toka mashariki, ukavuma juu ya nchi mchana kutwa na usiku kucha. Kulipokucha, ule upepo ukawa umeleta nzige.

14. Hao nzige wakaenea kila mahali nchini Misri, wakatua juu ya ardhi yote. Nzige hao walikuwa kundi kubwa kupindukia, kiasi ambacho hakijapata kutokea wala hakitatokea tena.

15. Waliifunika nchi yote ya Misri, hata ardhi ikaonekana kuwa giza. Walikula mimea yote na matunda yote yaliyosalia wakati wa ile mvua ya mawe. Hakuna hata jani moja lililosalia nchini. Hakuna jani lolote lililosalia juu ya miti wala mimea popote katika nchi yote ya Misri.

16. Hapo Farao akawaita Mose na Aroni kwa haraka, akawaambia, “Nimetenda dhambi dhidi ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, na dhidi yenu.

17. Kwa hiyo sasa ninawasihi mnisamehe dhambi yangu, mara hii moja tu, mkaniombee kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, aniondolee kifo hiki.”

18. Basi, Mose akaondoka kwa Farao, akaenda kumwomba Mwenyezi-Mungu.

19. Naye Mwenyezi-Mungu akaleta upepo mkali toka magharibi, ukawainua wale nzige na kuwasukumia kwenye bahari ya Shamu. Hakuna hata nzige mmoja aliyebaki katika nchi nzima ya Misri.

20. Lakini Mwenyezi-Mungu akamfanya Farao kuwa mkaidi, naye hakuwaachia Waisraeli waondoke.

21. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Nyosha mkono wako juu mbinguni ili giza nene litokee nchini Misri, giza nene ambalo mtu ataweza kulipapasa.”

22. Basi, Mose akanyosha mkono wake juu mbinguni, kukawa na giza nene kote nchini Misri kwa muda wa siku tatu.

23. Watu hawakuweza kuonana wala kuondoka mahali walipokuwa kwa muda huo wa siku tatu. Lakini Waisraeli wote walikuwa na mwanga huko Gosheni walimokuwa wanakaa.

24. Kisha, Farao akamwita Mose, akamwambia, “Nendeni mkamtumikie Mwenyezi-Mungu. Watoto wenu pia wanaweza kwenda pamoja nanyi. Lakini kondoo na mbuzi, na ng'ombe wenu wabaki.”

25. Lakini Mose akamwambia, “Ni lazima uturuhusu kuchukua wanyama wa tambiko na sadaka za kuteketezwa ili tukamtambikie Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu.

26. Ngombe wetu ni lazima pia tuwachukue wala hakuna hata ukwato mmoja utakaobaki nyuma, kwa sababu kutoka katika mifugo yetu wenyewe, tutamtumikia Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, wala sisi hatujui ni mnyama yupi tutakayemtolea Mwenyezi-Mungu tambiko mpaka tutakapofika huko.”

27. Lakini Mwenyezi-Mungu akamfanya Farao kuwa mkaidi, akakataa kuwaachia Waisraeli waondoke.

28. Farao akamwambia Mose, “Toka mbele yangu. Jihadhari sana. Usije kuniona tena, maana siku utakapokuja tena mbele yangu, utakufa!”

29. Mose naye akamwambia, “Sawa! Kama ulivyosema sitakuja kukuona tena.”

Kusoma sura kamili Kutoka 10