Agano la Kale

Agano Jipya

Kutoka 10:1-13 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Nenda kwa Farao. Mimi nimemfanya kuwa mkaidi na maofisa wake ili nipate kutenda ishara hizi miongoni mwao,

2. ili nyinyi mpate kuwasimulia watoto wenu na wajukuu wenu, jinsi nilivyowadhihaki Wamisri kwa kuzifanya ishara hizo miongoni mwao. Hivyo mtatambua kuwa mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.”

3. Basi, Mose na Aroni wakamwendea Farao na kumwambia, “Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Waebrania, anasema hivi, ‘Mpaka lini utakataa kujinyenyekesha mbele yangu? Waache watu wangu waondoke ili wapate kunitumikia.

4. Ukikataa kuwaacha watu wangu waondoke, basi, kesho nitaleta nzige waivamie nchi yako.

5. Nchi yote ya Misri itakuwa giza kwa sababu ya nzige hao. Watakula kila kitu kilichosalimika baada ya ile mvua ya mawe; pia hawataacha chochote juu ya miti inayoota mashambani.

6. Nzige hao watajaa katika nyumba zako, nyumba za maofisa wako na za Wamisri wote; watakuwa wengi kiasi ambacho hata wazee wenu hawajapata kuona tangu walipozaliwa, hadi leo.’” Basi, Mose akatoka kwa Farao.

7. Viongozi wa Farao wakamwuliza, “Je, mtu huyu atatusumbua mpaka lini? Waache watu hawa waende zao wakamtumikie Mwenyezi-Mungu, Mungu wao. Je, hujali kwamba nchi ya Misri inaangamia?”

8. Hapo, Mose na Aroni wakaitwa warudi kwa Farao, naye akawaambia, “Nendeni mkamtumikie Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Lakini, nauliza: Ni kina nani watakaokwenda pamoja nanyi?”

9. Mose akamjibu, “Kila mtu: Vijana na wazee, tutaondoka na watoto wetu wa kiume na wa kike, kondoo na mbuzi wetu na ng'ombe; kwa maana ni lazima tumfanyie sikukuu Mwenyezi-Mungu.”

10. Kwa kuwapuuza, Farao akawaambia, “Ehe! Mwenyezi-Mungu awe nanyi kama nitawaruhusu kamwe mwende zenu na watoto wenu. Ni dhahiri kwamba mnayo nia mbaya moyoni mwenu.

11. La hasha! Ni wanaume tu watakaokwenda kumtumikia Mwenyezi-Mungu, maana hilo ndilo mnalotaka.” Hapo Mose na Aroni wakafukuzwa mbele ya Farao.

12. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Nyosha mkono wako juu ya nchi ya Misri, nzige watokee ili waingie na kula mimea yote nchini na vyote vilivyosazwa na ile mvua ya mawe.”

13. Basi, Mose akainyosha fimbo yake juu ya nchi ya Misri. Mwenyezi-Mungu akaleta upepo toka mashariki, ukavuma juu ya nchi mchana kutwa na usiku kucha. Kulipokucha, ule upepo ukawa umeleta nzige.

Kusoma sura kamili Kutoka 10