Agano la Kale

Agano Jipya

Kutoka 1:13-22 Biblia Habari Njema (BHN)

13. Basi, Wamisri wakawatumikisha Waisraeli kikatili,

14. wakayafanya maisha yao kuwa magumu kwa kazi ngumu ya kutengeneza chokaa na kufyatua matofali, na kazi zote za shambani. Katika kazi hizo zote, Waisraeli walitumikishwa kwa ukatili.

15. Kisha, mfalme wa Misri akawaambia wakunga wa Misri, Shifra na Pua, ambao waliwahudumia wanawake wa Kiebrania,

16. “Mnapowahudumia wanawake wa Kiebrania wanapojifungua, ikiwa mtoto anayezaliwa ni wa kiume, muueni. Lakini ikiwa ni wa kike, mwacheni aishi.”

17. Lakini kwa kuwa wakunga hao walimcha Mungu, hawakufanya kama walivyoamriwa na mfalme wa Misri, bali waliwaacha watoto wa kiume wa Waisraeli waishi.

18. Basi, mfalme wa Misri akawaita wakunga hao, akawauliza, “Kwa nini mmefanya hivyo? Mbona mmewaacha watoto wa kiume waishi?”

19. Wao wakamjibu Farao, “Wanawake wa Kiebrania si sawa na wanawake wa Misri. Wao ni hodari; kabla mkunga hajafika, wao huwa wamekwisha jifungua.”

20. Basi, Mungu akawajalia mema wakunga hao, nao Waisraeli wakazidi kuongezeka na kuwa na nguvu sana.

21. Na kwa vile wakunga hao walimcha Mungu, Mungu akawajalia kupata jamaa zao wenyewe.

22. Kisha Farao akawaamuru watu wake wote hivi, “Kila mtoto wa kiume atakayezaliwa kwa Waebrania mtupeni mtoni Nili. Lakini kila mtoto wa kike, mwacheni aishi.”

Kusoma sura kamili Kutoka 1