Agano la Kale

Agano Jipya

Kumbukumbu La Sheria 6:8-17 Biblia Habari Njema (BHN)

8. Yafungeni katika mikono yenu na kuyavaa katika vipaji vya nyuso zenu kama ukumbusho.

9. Yaandikeni kwenye miimo ya milango yenu na malango ya miji yenu.

10. “Kama vile Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, alivyowaapia babu zenu, Abrahamu, Isaka na Yakobo, yeye atawapeni nchi yenye miji mikubwa na mizuri iliyostawi ambayo nyinyi hamkuijenga.

11. Nyumba zitakuwa zimejaa vitu vizuri ambavyo nyinyi hamkuviweka, kutakuwa na visima ambavyo hamkuvichimba na mashamba ya mizabibu na mizeituni ambayo hamkuyapanda. Mwenyezi-Mungu atakapowapeleka kwenye nchi hiyo ambako mtakuwa na chakula chote mnachohitaji,

12. hakikisheni kwamba hamtamsahau Mwenyezi-Mungu aliyewatoa Misri ambako mlikuwa watumwa.

13. Mtamcha Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, mtamtumikia yeye peke yake na kuapa kwa jina lake peke yake.

14. Msiabudu miungu mingine, miungu ya watu walio jirani nanyi,

15. hasira ya Mwenyezi-Mungu isije ikawaka juu yenu, naye akawafutilia mbali kutoka duniani, maana Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu aliye kati yenu, ni Mungu mwenye wivu.

16. “Msimjaribu Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kama mlivyomjaribu kule Masa.

17. Hakikisheni kwamba mnazitii amri zake Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, maamuzi na masharti yake ambayo amewaamuru.

Kusoma sura kamili Kumbukumbu La Sheria 6