Agano la Kale

Agano Jipya

Kumbukumbu La Sheria 31:11-27 Biblia Habari Njema (BHN)

11. wakati watu wa Israeli wanapokuja mbele ya Mwenyezi-Mungu mahali pale atakapochagua mtawasomea watu wote wa Israeli sheria hii.

12. Wakusanye watu: Wanaume, wanawake, watoto na wageni wanaoishi katika miji yenu, ili kila mmoja asikie maneno haya ya kujifunza kumcha Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, na kuwa waangalifu kutekeleza maneno ya sheria hii.

13. Nao wazawa wao ambao hawajasikia sheria ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, wapate kuisikia na kujifunza kumcha Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, muda wote mtakaoishi katika nchi ambayo mnakwenda kuimiliki ngambo ya mto Yordani.”

14. Basi, Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Siku yako ya kuaga dunia imekaribia. Mwite Yoshua, mje pamoja katika hema la mkutano ili nimpe maagizo.” Basi, Mose na Yoshua wakaenda katika hema la mkutano,

15. naye Mwenyezi-Mungu akawatokea humo katika nguzo ya wingu ambayo ilisimama kwenye mlango wa hema.

16. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Umekaribia sasa kuaga dunia, na baada ya kufariki, watu wataanza kuniacha na kuiendea miungu mingine ya nchi hiyo ambamo watakwenda kuishi; wataniacha na kuvunja agano nililoagana nao.

17. Hapo hasira yangu itawawakia siku hiyo, nami nitawaacha na kuuficha uso wangu mbali nao, wataangamizwa. Maovu mengi na taabu zitawavamia hata watambue kwamba maovu hayo yamewapata kwa kuwa Mungu wao hayupo miongoni mwao.

18. Hakika nitawaficha uso wangu kwa sababu wamefanya mambo maovu na kuigeukia miungu mingine.

19. “Sasa, andika wimbo huu, uwafundishe watu wa Israeli ili uwe ushahidi wangu juu yao.

20. Nitakapowapeleka katika nchi inayotiririka maziwa na asali, kama nilivyowaapia babu zao, nao wakala wakashiba na kunenepa, wataigeukia miungu mingine na kuitumikia; watanidharau na kulivunja agano langu.

21. Watakapovamiwa na maafa mengi na taabu, wimbo huu utawakabili kama ushahidi kwani hautasahauliwa na wazawa wao. Na hata sasa, kabla sijawapeleka katika nchi niliyoapa kuwapa, naijua mipango ambayo wanapanga.”

22. Basi, Mose aliandika wimbo huo siku hiyohiyo, akawafundisha Waisraeli.

23. Kisha Mwenyezi-Mungu akamwagiza Yoshua, mwana wa Nuni, akamwambia, “Uwe imara na hodari, maana utawaongoza Waisraeli katika nchi ambayo nimewaapia kuwapa, nami nitakuwa pamoja nawe.”

24. Mose alipomaliza kuandika maneno ya sheria hiyo tangu mwanzo mpaka mwisho,

25. aliwaambia Walawi, waliokuwa na jukumu la kubeba lile sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu,

26. “Chukueni kitabu hiki cha sheria, mkiweke karibu na sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ili kiwe ushahidi dhidi yenu.

27. Maana najua mlivyo waasi na wakaidi. Ikiwa mmemwasi Mwenyezi-Mungu wakati niko hai pamoja nanyi, itakuwaje baada ya kifo changu?

Kusoma sura kamili Kumbukumbu La Sheria 31