Agano la Kale

Agano Jipya

Kumbukumbu La Sheria 31:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Mose aliendelea kuongea na Waisraeli wote,

2. akawaambia, “Mimi sasa nina umri wa miaka 120, na sina nguvu ya kufanya kazi zaidi. Tena Mwenyezi-Mungu, ameniambia kuwa sitavuka mto Yordani.

3. Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atawatangulia na kuyaangamiza mataifa yanayoishi huko, ili muimiliki nchi yao. Yoshua atakuwa kiongozi wenu kama alivyosema Mwenyezi-Mungu.

4. Mwenyezi-Mungu atayaangamiza mataifa hayo kama vile alivyowaangamiza Sihoni na Ogu, wafalme wa Waamori, na nchi yao.

5. Mwenyezi-Mungu atawapeni ushindi juu yao nanyi mtawatendea kama nilivyowaamuru.

6. Muwe imara na hodari, wala msiwaogope au kutishwa nao, maana Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu ndiye anayekwenda pamoja nanyi. Yeye hataacha kuwasaidia na hatawatupa.”

7. Kisha Mose akamwita Yoshua, akamwambia mbele ya watu wote wa Israeli, “Uwe Imara na hodari, maana wewe utawaongoza watu hawa kwenda kuimiliki nchi ambayo Mwenyezi-Mungu aliwaahidi babu zao; nawe utawakabidhi waimiliki.

8. Mwenyezi-Mungu ndiye anayewaongoza; yeye atakuwa pamoja nanyi; yeye hataacha kuwasaidia na hatawatupa. Hivyo, msiogope wala msifadhaike.”

9. Basi, Mose aliandika sheria hiyo, akawapa makuhani wa ukoo wa Lawi ambao walikuwa na jukumu la kubeba agano la Mwenyezi-Mungu, na wazee wote wa Israeli.

10. Kisha akawaamuru akasema, “Kila mwaka wa saba utakuwa mwaka wa mafungulio. Katika sikukuu ya vibanda, mwaka huo,

11. wakati watu wa Israeli wanapokuja mbele ya Mwenyezi-Mungu mahali pale atakapochagua mtawasomea watu wote wa Israeli sheria hii.

12. Wakusanye watu: Wanaume, wanawake, watoto na wageni wanaoishi katika miji yenu, ili kila mmoja asikie maneno haya ya kujifunza kumcha Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, na kuwa waangalifu kutekeleza maneno ya sheria hii.

Kusoma sura kamili Kumbukumbu La Sheria 31