Agano la Kale

Agano Jipya

Kumbukumbu La Sheria 22:4-18 Biblia Habari Njema (BHN)

4. “Ukiona punda au ng'ombe wa nduguyo ameanguka njiani, usiache kumsaidia nduguyo; utamsaidia kumwinua.

5. “Wanawake wasivae nguo za wanaume, na wanaume wasivae nguo za wanawake. Anayefanya hivyo ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.

6. “Ukikuta kiota cha ndege mtini au njiani, kina makinda au mayai na mamandege ameyafunika hayo makinda au mayai, usimchukue mamandege na makinda yake.

7. Utamwacha mamandege aende zake, lakini unaweza kuchukua makinda. Ukifanya hivyo utafanikiwa na kuishi maisha marefu.

8. “Unapojenga nyumba, jenga ukingo pembeni mwa paa, usije ukalaumiwa kama mtu akianguka kutoka huko, akafa.

9. “Usipande mizabibu yako pamoja na mimea mingine, la sivyo mazao yote yatakuwa haramu, siyo tu yale uliyopanda bali pia matunda ya mizabibu.

10. “Usilime shamba kwa kutumia ng'ombe na punda pamoja.

11. “Usivae mavazi yaliyofumwa kwa sufu na kitani.

12. “Funga vishada katika pembe nne za vazi lako.

13. “Mwanamume akioa mwanamke, halafu baadaye akate shauri kumwacha,

14. na kumshtaki kwamba ametenda mambo ya aibu, na kumharibia sifa kwa kusema kwamba hakupata ushahidi wa ubikira wakati alipomwoa,

15. basi, wazazi wa mwanamke huyo watachukua ushahidi wa ubikira wa binti yao kwa wazee kwenye lango la mji na kuwaambia,

16. ‘Tulimwoza binti yetu kwa mtu huyu, lakini sasa hamtaki tena,

17. na ajabu ni kwamba amemshtaki mambo ya aibu na kusema ati hakumkuta na ushahidi wowote wa ubikira. Hata hivyo ushahidi wa ubikira wa binti yetu ni huu.’ Halafu atakunjua nguo yenye huo ushahidi mbele ya wazee wa mji.

18. Hapo wazee wa mji watamchukua yule mwanamume na kumpiga viboko.

Kusoma sura kamili Kumbukumbu La Sheria 22