Agano la Kale

Agano Jipya

Kumbukumbu La Sheria 2:21-33 Biblia Habari Njema (BHN)

21. Walikuwa watu wengi, wenye nguvu na warefu kama Waanaki. Lakini Mwenyezi-Mungu aliwaangamiza walipofika Waamori ambao walichukua nchi yao wakaishi humo badala yao.

22. Mwenyezi-Mungu alifanya kama alivyowafanyia wazawa wa Esau, Waedomu, ambao wanaishi katika nchi ya Seiri. Aliwaangamiza Wahori wakati Waedomu walipofika huko, wakainyakua nchi yao na kuishi humo hadi leo.

23. Waavi walikuwa hapo awali wakiishi katika vijiji vya mwambao wa Mediteranea mpaka Gaza. Wakaftori kutoka kisiwa cha Kaptori wakawaangamiza, wakaishi humo badala yao).

24. “Kisha Mwenyezi-Mungu alituamuru: ‘Haya! Anzeni safari. Vukeni bonde la Arnoni. Mimi nimemtia mikononi mwenu Sihoni, mfalme wa Waamori wa Heshboni na nchi yake. Mshambulieni na kuanza kuimiliki nchi yake.

25. Leo nitaanza kuwafanya watu wote duniani wawe na woga na hofu juu yenu; watasikia habari zenu nao watatetemeka na kufadhaika.’

26. “Basi, nikatuma watu kutoka jangwa la Kedemothi waende kwa mfalme Sihoni wa Heshboni na ujumbe ufuatao wa amani:

27. ‘Turuhusu tupite katika nchi yako. Tutapitia barabarani na kwenda moja kwa moja bila kugeuka kulia wala kushoto.

28. Chakula chetu tutakinunua kwako na maji ya kunywa pia. Tunachoomba tu ni ruhusa ya kupita kwa miguu nchini mwako,

29. tuvuke mto Yordani na kuingia katika nchi ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu anatupatia. Wazawa wa Esau wanaoishi Seiri na Wamoabu waishio Ari walituruhusu pia kupita katika nchi yao’.

30. “Lakini Sihoni, mfalme wa Heshboni, hakuturuhusu tupite nchini mwake. Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, alimfanya awe na kichwa kigumu na mkaidi wa moyo, ili tumshinde na kuchukua nchi yake ambayo tunaimiliki hadi leo.

31. “Halafu Mwenyezi-Mungu akaniambia, ‘Tazama, nimeanza kumtia mfalme Sihoni na nchi yake mikononi mwenu; anzeni kuichukua nchi yake na kuimiliki’.

32. Kisha Sihoni alitoka na watu wake wote kupigana nasi karibu na mji wa Yahasa.

33. Naye Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, akamtoa, tukamshinda yeye, watoto wake na watu wake wote.

Kusoma sura kamili Kumbukumbu La Sheria 2