Agano la Kale

Agano Jipya

Kumbukumbu La Sheria 18:3-15 Biblia Habari Njema (BHN)

3. “Na hii itakuwa haki ya makuhani kutoka kwa watu wanaotoa sadaka iwe ni ng'ombe au kondoo: Watampa kuhani mguu wa mbele, mashavu na matumbo.

4. Mtawapa sehemu ya kwanza ya mazao yenu ya nafaka, divai, mafuta yenu na sufu ya kwanza ya kondoo wenu.

5. Katika makabila yenu yote, Mwenyezi-Mungu amechagua kabila la Walawi limtumikie kama makuhani milele.

6. “Ikiwa Mlawi yeyote atapenda mwenyewe anaweza kutoka mji wowote ule wa Israeli kwenda pale mahali Mwenyezi-Mungu alipochagua,

7. na hapo anaweza kuhudumu kwa jina la Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, kama wale Walawi wengine wanaohudumu mbele ya Mwenyezi-Mungu.

8. Watapata mafungu yao sawa ya kula, ingawa wanayo mapato kutokana na mauzo ya mali za jamaa zao.

9. “Mtakapofika katika ile nchi ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu atawapa, msifuate desturi za kuchukiza za mataifa hayo.

10. Pasiwe mtu yeyote miongoni mwenu atakayemtambika mtoto wake wa kiume au wa kike kwa moto, wala mtu apigaye ramli, wala mwaguzi, wala mpiga bao,

11. wala mchawi, wala mlozi, wala mwenye kutaka kauli kwa mizimu na pepo au kutoka kwa wafu.

12. Maana yeyote atendaye mambo haya ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu; na kwa ajili ya mambo haya ya kuchukiza, Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, anawafukuza watu wa namna hiyo mbele yenu.

13. Muwe wakamilifu mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.

14. “Mataifa haya ambayo mtaimiliki nchi yao hufuata maongozi ya waaguzi na wapiga ramli; lakini Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu hawaruhusu nyinyi kufanya hivyo.

15. “Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu atawateulieni nabii aliye kama mimi kutoka miongoni mwenu, nanyi mtamsikiliza huyo.

Kusoma sura kamili Kumbukumbu La Sheria 18