Agano la Kale

Agano Jipya

Kumbukumbu La Sheria 16:9-22 Biblia Habari Njema (BHN)

9. “Mtahesabu majuma saba; mtaanza kuyahesabu tangu mnapoanza kuvuna nafaka.

10. Halafu mtaadhimisha sikukuu ya majuma kwa heshima ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kwa kutoa sadaka ya hiari, mtakayotoa kadiri awabarikiavyo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.

11. Mtafurahia mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, nyinyi pamoja na wana wenu na binti zenu, watumishi wenu, Walawi, wageni, yatima na wajane ambao wanaishi pamoja nanyi. Fanyeni haya katika mahali Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atakapochagua likae jina lake.

12. Mkumbuke kuwa mlikuwa watumwa kule Misri; basi muwe waangalifu kufuata masharti haya.

13. “Baada ya kupura nafaka yenu yote na kukamua zabibu zenu, adhimisheni sikukuu ya vibanda kwa muda wa siku saba.

14. Mtafanya sherehe hiyo, nyinyi na watoto wenu wa kiume na wa kike, watumishi wenu, Walawi, wageni, yatima na wajane ambao huishi katika miji yenu.

15. Kwa siku saba mtamfanyia Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, sherehe mahali ambapo Mwenyezi-Mungu atapachagua; kwa sababu Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu atawabariki kwa mazao yenu yote na katika shughuli zenu zote nanyi hakika mtafurahi.

16. “Wanaume wote wa taifa lenu watakuja mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, mara tatu kila mwaka, mahali atakapopachagua: Wakati wa sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu, sikukuu ya kuvuna majuma na wakati wa sikukuu ya vibanda. Wasiende mbele ya Mwenyezi-Mungu mikono mitupu.

17. Wote watatoa kadiri wanavyoweza kulingana na baraka Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, alizowajalia.

18. “Mtateua waamuzi na maofisa kutoka makabila yenu katika miji yenu ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atawapa, nao watatoa hukumu za haki kwa watu.

19. Msipotoshe haki; msiwe na upendeleo, wala msikubali kupokea rushwa, kwa kuwa rushwa hupofusha macho ya watu wenye hekima na kupotosha kesi ya mtu mwadilifu.

20. Mtazingatia haki tu, ili mpate kuishi na kuimiliki nchi mnayopewa na Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.

21. “Msipande mti wowote uwe nguzo ya mungu wa uongo karibu na meza ya madhabahu sadaka mtakayomjengea Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.

22. Wala msisimamishe nguzo ambayo Mwenyezi-Mungu Mungu wako anaichukia.

Kusoma sura kamili Kumbukumbu La Sheria 16