Agano la Kale

Agano Jipya

Kumbukumbu La Sheria 12:11-28 Biblia Habari Njema (BHN)

11. basi huko mahali Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atakapochagua ili jina lake likae, hapo ndipo mtakapopeleka kila kitu ninachowaamuru: Tambiko zenu za kuteketeza na sadaka zenu, zaka zenu na matoleo yenu, na sadaka zenu za nadhiri mnazoahidi kumtolea Mwenyezi-Mungu.

12. Huko mtafurahi mbele yake Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, nyinyi pamoja na watoto wenu wa kiume na wa kike, watumishi wenu wa kiume na wa kike, na Walawi wanaoishi katika miji yenu, maana wao hawana sehemu wala urithi kati yenu.

13. Jihadharini msitoe sadaka zenu za kuteketezwa mahali popote mnapopaona;

14. bali katika mahali atakapopachagua Mwenyezi-Mungu katika mojawapo ya makabila yenu. Hapo ndipo mtakapotoa sadaka zenu za kuteketezwa, na ndipo mtakapofanyia mambo yote niliyowaamuru.

15. “Lakini mna uhuru wa kuchinja na kula wanyama wenu popote katika makao yenu mnavyopenda, kama baraka za Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, alizowapa, kadiri mtakavyojaliwa na Mwenyezi-Mungu. Watu wote, walio safi au najisi wanaweza kula nyama hizo, kama vile mlavyo nyama ya paa au ya kulungu.

16. Lakini msile damu ya wanyama hao; imwageni damu hiyo ardhini kama maji.

17. Msile vitu vifuatavyo mahali mnapoishi: Zaka ya nafaka zenu, wala ya divai yenu, wala ya mafuta yenu, wala ya wazaliwa wa kwanza wa ng'ombe au kondoo wenu, wala sadaka zenu za nadhiri au tambiko zenu za hiari, wala matoleo mengineyo.

18. Mtavila vitu hivyo mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, mahali atakapopachagua Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Mtavila nyinyi pamoja na watoto wenu wa kiume na wa kike, watumishi wenu wa kiume na wa kike, na Walawi wanaoishi katika miji yenu.

19. Pia hakikisheni kwamba hamtawasahau Walawi muda wote mtakaoishi katika nchi yenu.

20. “Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atakapoipanua nchi yenu, kama alivyoahidi, nanyi mtasema, ‘Tutakula nyama’, kwa vile mnapenda kula nyama, mnaweza kula nyama kiasi chochote mnachotaka.

21. Basi, mahali atakapochagua Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, aweke jina lake, hapo mnaweza kuchinja ng'ombe au kondoo yeyote ambaye Mwenyezi-Mungu amewajalia, kama nilivyowaamuru, na mnaweza kula kiasi chochote mnachotaka cha nyama hiyo, kama mkiwa katika miji yenu.

22. Mtaila nyama hiyo kama aliwavyo paa au kulungu. Mtu yeyote anaweza kula, aliye safi na asiye safi.

23. Ila hakikisheni kwamba hamli damu, maana damu ni uhai; hivyo basi, msile uhai pamoja na nyama.

24. Msile damu hiyo, bali imwageni chini kama maji.

25. Msile damu, nanyi mtafanikiwa pamoja na wazawa wenu, maana mtakuwa mnatenda mema mbele ya Mwenyezi-Mungu.

26. Vitu vitakatifu mtakavyotoa na sadaka zenu za nadhiri, mtavichukua na kuvipeleka mahali Mwenyezi-Mungu atakapochagua.

27. Hapo, mtatoa sadaka za kuteketezwa, nyama na damu, kwenye madhabahu ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu; damu ya mnyama mtainyunyiza kwenye madhabahu yake Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, lakini mnaruhusiwa kula nyama.

28. Jihadharini kutii maneno haya niliyowaamuru, ili mpate kufanikiwa nyinyi pamoja na wazawa wenu baada yenu milele, maana mtakuwa mnatenda yaliyo mema na yaliyo sawa mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.

Kusoma sura kamili Kumbukumbu La Sheria 12