Agano la Kale

Agano Jipya

Kumbukumbu La Sheria 11:7-18 Biblia Habari Njema (BHN)

7. Maana macho yenu yameona matendo yote haya makubwa ambayo Mwenyezi-Mungu aliyafanya.

8. “Tiini amri zote ninazowaamuru siku hii ya leo, ili muweze kuingia na kuimiliki nchi mnayoiendea,

9. mpate kuishi kwa muda mrefu katika nchi hiyo inayotiririka maziwa na asali; nchi ambayo Mwenyezi-Mungu aliahidi kuwapa babu zenu na wazawa wao.

10. Kwa kuwa nchi mnayokwenda kuimiliki si kama nchi ya Misri mlikotoka, ambako mlipanda nafaka, mkamwagilia maji kwa miguu kama mashamba ya mboga.

11. Lakini nchi mnayokwenda kuimiliki, ni nchi ya milima na mabonde, nchi ambayo hupata maji ya mvua kutoka mbinguni,

12. nchi ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, huitunza; Mwenyezi-Mungu huiangalia daima tangu mwanzo wa mwaka hadi mwisho wa mwaka.

13. “Basi, mkizitii amri zangu ninazowapeni leo, mkampenda Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, mkamtumikia kwa moyo wenu wote na kwa roho yenu yote,

14. yeye ataipatia mvua nchi yenu wakati wake, mvua za masika na mvua za vuli, nanyi mtavuna nafaka yenu, divai yenu na mafuta yenu.

15. Ataotesha majani mashambani kwa ajili ya ng'ombe wenu, nanyi mtakula na kushiba.

16. Jihadharini, mioyo yenu isije ikadanganywa, mkageuka na kuitumikia miungu mingine na kuiabudu,

17. nayo hasira ya Mwenyezi-Mungu ikawaka dhidi yenu, akazifunga mbingu hata pasiwepo mvua na nchi ikaacha kutoa mazao yake, halafu mkaangamia upesi kutoka katika nchi nzuri ambayo Mwenyezi-Mungu anawapa.

18. “Yawekeni maneno yangu haya mioyoni mwenu na rohoni mwenu. Yafungeni mikononi mwenu kama alama na kuyavaa katika paji la uso.

Kusoma sura kamili Kumbukumbu La Sheria 11