Agano la Kale

Agano Jipya

Isaya 8:1-16 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Mwenyezi-Mungu aliniambia hivi: “Chukua ubao mkubwa, uandike juu yake maneno yanayosomeka kwa urahisi: ‘TEKA-HARAKA-POKONYA-UPESI.’”

2. Basi, nikajipatia mashahidi wawili waaminifu ambao wangenishuhudia: Kuhani Uria na Zekaria, mwana wa Yeberekia.

3. Nililala na mke wangu ambaye pia ni nabii, akapata mimba, akajifungua mtoto wa kiume. Mwenyezi-Mungu akaniambia, “Mpe mtoto huyo jina ‘Teka-haraka-pokonya-upesi.’

4. Maana kabla mtoto huyu hajafikia umri wa kuweza kutamka: ‘Baba’ au ‘Mama,’ utajiri wa Damasko na nyara walizoteka huko Samaria zitapelekwa kwa mfalme wa Ashuru.”

5. Mwenyezi-Mungu aliongea nami tena, akaniambia,

6. “Kwa kuwa watu hawa wameyakataa maji ya Shiloa yatiririkayo polepole, wakafa moyo mbele ya mfalme Resini na mfalme Peka mwana wa Remalia,

7. basi, mimi Bwana nitawaletea mafuriko makuu ya maji ya mto Eufrate yaani mfalme wa Ashuru na nguvu zake zote; yatafurika na kupita kingo zake.

8. Utaingia nchini Yuda kwa nguvu na kufurika na kupanda mpaka shingoni; utaenea juu ya nchi yako yote, ee Emanueli!”

9. Unganeni enyi watu wa mataifa nanyi mtafedheheshwa!Sikilizeni enyi nchi za mbali duniani!Jiwekeni tayari na kufedheheshwa;naam, kaeni tayari na kufedheheshwa.

10. Shaurianeni pamoja lakini itakuwa bure;fanyeni mipango lakini haitafaulu,maana Mungu yu pamoja nasi.

11. Mwenyezi-Mungu alinionya kwa nguvu nisifuate njia za watu hawa, akaniambia,

12. “Usijumuike nao katika njama zao, wala usiogope yale wanayoyaogopa wala kuwa na hofu.

13. Nitambue mimi peke yangu, Mwenyezi-Mungu wa majeshi, kuwa mtakatifu; utaniogopa na kunicha mimi peke yangu.

14. Mimi nitakuwa kimbilio, nitakuwa pia kama jiwe la kujikwaa, mwamba wa kuziangusha falme za Israeli na Yuda; nitakuwa mtego wa kuwatega na kuwanasa wakazi wa Yerusalemu.

15. Watu wengi watajikwaa, wataanguka na kupondeka; watanaswa katika mtego huo na kuchukuliwa mateka.”

16. Nitalihifadhi agizo hilo na kulifunga fundisho hilo miongoni mwa wafuasi wangu.

Kusoma sura kamili Isaya 8