Agano la Kale

Agano Jipya

Isaya 7:13-25 Biblia Habari Njema (BHN)

13. Basi, Isaya akamjibu, “Sikiliza basi, enyi watu wa ukoo wa Daudi! Je, haitoshi kuwachosha watu hata sasa mnataka kumchosha Mungu wangu pia?

14. Haya basi, Bwana mwenyewe atawapa ishara: Msichana atachukua mimba, atajifungua mtoto wa kiume na kumwita jina lake Emanueli.

15. Atakula siagi na asali mpaka atakapojua kukataa mabaya na kuchagua mema.

16. Maana, kabla mtoto huyo hajajua kukataa maovu na kuchagua mema, nchi za wafalme hao wawili unaowaogopa zitakuwa mahame.

17. Mwenyezi-Mungu atakuletea wewe pamoja na watu wako na jamii yote ya kifalme siku za taabu kuliko zile zote zilizowahi kutokea tangu wakati watu wa Efraimu walipojitenga na Yuda; yaani, atawaleteeni mfalme wa Ashuru.”

18. Wakati huo, Mwenyezi-Mungu atawapigia mruzi watu wa Misri waje kama nzi toka vijito vya mto Nili; na watu wa Ashuru waje kama nyuki kutoka nchi yao.

19. Watakuja makundi kwa makundi na kuyajaza mabonde yaliyopasukapasuka, mapango miambani, miiba, vichaka vyote na malisho yote.

20. Wakati huo, Bwana atakopa wembe kutoka ngambo ya mto Eufrate, yaani mfalme wa Ashuru. Atawanyoa vichwa vyenu, miili yenu na kukatilia mbali pia ndevu zenu.

21. Wakati huo, mtu atafuga ng'ombe mmoja mchanga na kondoo wawili;

22. nao watatoa maziwa kwa wingi hata aweze kula siagi. Watu watakaosalia katika nchi watakula siagi na asali.

23. Wakati huo, kila mahali palipokuwa na mashamba ya mizabibu kwa maelfu ya thamani ya fedha 1,000 kwa kipimo cha hekalu yatakuwa mbigili na miiba mitupu.

24. Watu watakwenda huko kuwinda kwa pinde na mishale, maana nchi yote itakuwa imejaa mbigili na miiba.

25. Nayo milima yote iliyokuwa ikilimwa itakuwa imejaa mbigili na miiba, hata hakuna mtu atakayejaribu kwenda huko, badala yake itakuwa malisho ya ng'ombe na kondoo.

Kusoma sura kamili Isaya 7