Agano la Kale

Agano Jipya

Isaya 59:3-16 Biblia Habari Njema (BHN)

3. Maana mikono yenu imetiwa najisi kwa mauaji,na vidole vyenu kwa matendo maovu.Midomo yenu imesema uongo,na ndimi zenu husema uovu.

4. Hakuna atoaye madai yake kwa haki,wala anayeshtaki kwa uaminifu.Mnategemea hoja batili;mnasema uongo.Mnatunga hila na kuzaa uovu.

5. Mnaangua mayai ya joka lenye sumu,mnafuma utando wa buibui.Anayekula mayai yenu hufa,na yakipasuliwa nyoka hutokea.

6. Utando wenu haufai kwa mavazi,watu hawawezi kujifunikia mnachofuma.Kazi zenu ni kazi za uovu,matendo yenu yote ni ukatili mtupu.

7. Mko mbioni kutenda maovu,mnaharakisha kumwaga damu isiyo na hatia.Mawazo yenu ni mawazo ya uovu,popote mwendapo mnaacha ukiwa na uharibifu.

8. Njia ya amani hamwijui kamwe;njia zenu zote ni za dhuluma.Mmejifanyia njia potovu,yeyote anayepitia humo hapati amani.

9. Ndio maana haki iko mbali nasi,maongozi ya uadilifu hayapo kwetu.Tunatazamia kupata mwanga kumbe ni giza tupu,twatazamia mwangaza, lakini twatembea gizani.

10. Kama vipofu twapapasapapasa ukuta;tunasitasita kama watu wasio na macho.Tunajikwaa mchana kana kwamba ni usiku,miongoni mwa wenye nguvu sisi ni kama wafu.

11. Twanguruma kama dubu,twaomboleza tena na tena kama hua.Twatazamia hukumu ya haki, lakini haipo,twatazamia wokovu, lakini uko mbali nasi.

12. Makosa yetu mbele yako ni mengi mno,dhambi zetu zashuhudia dhidi yetu.Naam, makosa yetu tunaandamana nayo,tunayajua maovu yetu.

13. Tumekuasi na kukukana ee Mwenyezi-Mungu,tumekataa kukufuata ewe Mungu wetu.Udhalimu na uasi ndivyo tunavyopania,mioyoni mwetu twatunga na kutoa maneno ya uongo.

14. Haki imewekwa kando,uadilifu uko mbali;ukweli unakanyagwa mahakamani,uaminifu haudiriki kuingia humo.

15. Ukweli umekosekana,naye anayeacha uovu hunyanyaswa.Mungu aliona mambo hayo, akachukizwa,alichukizwa kwamba hakuna haki.

16. Aliona kwamba hakuna mtu aliyejali,akashangaa kwamba hakuna aliyeingilia kati.Basi akaamua kunyosha mkono wake mwenyewe,uadilifu wake ukamhimiza.

Kusoma sura kamili Isaya 59