Agano la Kale

Agano Jipya

Hesabu 9:6-19 Biblia Habari Njema (BHN)

6. Lakini, baadhi ya watu waliokuwapo walikuwa hawawezi kuiadhimisha sikukuu hiyo ya Pasaka kwa sababu walikuwa wamegusa maiti, wakawa najisi. Hao waliwaendea Mose na Aroni,

7. wakawaambia, “Sisi tu najisi kwa kuwa tumegusa maiti, lakini kwa nini tukatazwe kumtolea Mwenyezi-Mungu sadaka zake kwa wakati uliopangwa pamoja na Waisraeli wengine?”

8. Mose akawajibu, “Ngojeni mpaka hapo nitakapopata maagizo juu yenu kutoka kwa Mwenyezi-Mungu.”

9. Naye Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose,

10. “Mmoja wenu au mmoja wa wazawa wenu akiwa najisi kwa sababu amegusa maiti au akiwa mbali safarini, lakini akiwa anataka kuiadhimisha sikukuu ya Pasaka,

11. mtu kama huyo anaruhusiwa kufanya hivyo mwezi mmoja baadaye, jioni ya siku ya kumi na nne ya mwezi wa pili. Ataiadhimisha kwa kula mikate isiyotiwa chachu na mboga chungu.

12. Wasibakize chakula chochote hadi asubuhi, wala wasivunje hata mfupa mmoja wa wanyama wa Pasaka. Wataiadhimisha sikukuu hii ya Pasaka kulingana na kanuni zake zote.

13. Lakini mtu yeyote ambaye ni safi au hayumo safarini, asipoiadhimisha sikukuu ya Pasaka, atatengwa na watu wake kwa kuwa hakunitolea sadaka kwa wakati uliopangwa. Ni lazima aadhibiwe kwa ajili ya dhambi yake.

14. “Ikiwa kuna mgeni anayeishi pamoja nanyi na anapenda kuiadhimisha sikukuu ya Pasaka, mtu huyo sharti afanye hivyo kulingana na masharti na maagizo yote ya Pasaka. Kila mtu atafuata masharti yaleyale, akiwa mgeni au mwenyeji.”

15. Siku ambayo hema takatifu lilisimikwa, wingu lilishuka na kulifunika hema la maamuzi. Wakati wa usiku wingu hilo lilionekana kama moto mpaka asubuhi.

16. Hivyo ndivyo ilivyokuwa kila siku; wingu lililifunika hema mchana, na usiku lilionekana kama moto.

17. Kila mara wingu hilo lilipoinuliwa juu ya hema, Waisraeli walivunja kambi na kupiga kambi tena mahali wingu hilo lilipotua.

18. Walisafiri kwa amri ya Mwenyezi-Mungu, na kupiga kambi tena kwa amri yake. Muda wote wingu hilo lilipokuwa juu ya hema, watu walikaa katika kambi hiyo.

19. Hata kama wingu hilo lilikaa juu ya hema kwa muda wa siku nyingi, Waisraeli walimtii Mwenyezi-Mungu, nao hawakuondoka.

Kusoma sura kamili Hesabu 9