Agano la Kale

Agano Jipya

Hesabu 6:5-16 Biblia Habari Njema (BHN)

5. “Siku zote za nadhiri yake ya kujitenga, hatanyoa nywele zake; mpaka muda wa nadhiri yake ya kujiweka wakfu kwa Mwenyezi-Mungu utakapomalizika, atakuwa mtakatifu, ataziacha nywele zake ziwe ndefu.

6. Siku zote atakazokuwa amejiweka wakfu kwa Mwenyezi-Mungu, mtu huyo asikaribie maiti,

7. hata kama ni ya baba, mama, ndugu au dada yake, asije akajitia unajisi kwa maana amejiweka wakfu kwa Mwenyezi-Mungu kwa kiapo.

8. Muda wote atakaokuwa mnadhiri atakuwa wakfu kwa Mwenyezi-Mungu.

9. “Endapo nywele za mnadhiri zitatiwa unajisi mtu afapo ghafla karibu naye, atakinyoa kichwa chake wakati wa siku ya kutakaswa kwake; atakinyoa katika siku ya saba.

10. Katika siku ya nane atapeleka hua wawili au makinda mawili ya njiwa kwa kuhani penye lango la hema la mkutano.

11. Kuhani atamtoa mmoja kuwa sadaka ya kuondoa dhambi na mwingine kuwa sadaka ya kuteketezwa, naye atamfanyia upatanisho, kwa sababu alitenda dhambi kwa ajili ya maiti. Siku hiyohiyo, atakiweka wakfu kichwa chake

12. na kujiweka wakfu kwa Mwenyezi-Mungu kwa siku zake za kujitenga. Hizo siku za kwanza hazitahesabiwa kwa sababu nywele zake zilizokuwa zimewekwa wakfu zimetiwa unajisi. Atatoa mwanakondoo dume wa mwaka mmoja kuwa sadaka ya hatia.

13. “Hii ndiyo sheria ya mnadhiri wakati akisha kamilisha muda wake wa kujiweka wakfu: Ataletwa penye lango la hema la mkutano,

14. na kumtolea Mwenyezi-Mungu zawadi zake: Mwanakondoo dume mmoja wa mwaka mmoja asiye na dosari kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa; mwanakondoo jike mmoja wa mwaka mmoja asiye na dosari kwa ajili ya sadaka ya kuondoa dhambi; na kondoo dume mmoja asiye na dosari kwa ajili ya sadaka ya amani.

15. Pia atatoa kikapu cha mikate isiyotiwa chachu: Maandazi ya unga laini na mafuta, na mikate myembamba iliyopakwa mafuta pamoja na sadaka za nafaka na za kinywaji.

16. “Kuhani atamtolea Mwenyezi-Mungu vitu vyote hivi pamoja na sadaka yake ya dhambi na sadaka yake ya kuteketezwa.

Kusoma sura kamili Hesabu 6