Agano la Kale

Agano Jipya

Hesabu 6:17-27 Biblia Habari Njema (BHN)

17. Atamtolea Mwenyezi-Mungu huyo kondoo kama tambiko ya amani, atamtoa pamoja na kikapu cha mikate isiyotiwa chachu, sadaka ya nafaka na ya kinywaji.

18. Hapo penye mlango wa hema la mkutano, mnadhiri huyo atanyoa nywele zake na kuzitia katika moto ulio chini ya tambiko ya sadaka ya amani.

19. “Kisha kuhani atachukua bega la yule kondoo dume likiwa limechemshwa pamoja na andazi moja lililotiwa chachu kutoka kikapuni na mikate myembamba pia isiyotiwa chachu na kumpa mnadhiri mikononi akisha maliza kunyoa nywele zake alizokuwa nazo wakati wa kuwekwa wakfu.

20. Halafu kuhani atavitikisa vitu hivyo kama sadaka ya kutikisa mbele ya Mwenyezi-Mungu; vyote hivi ni sehemu takatifu kwa kuhani, pamoja na kidari kilichotikiswa na paja lililotolewa kama sadaka. Baada ya hayo yote, mnadhiri anaweza kunywa divai.

21. “Hiyo ndizo sheria inayomhusu mnadhiri anayeahidi kwa kiapo. Sadaka yake kwa Mwenyezi-Mungu ilingane na nadhiri yake, licha ya chochote kingine anachoweza kutoa; atafanya kulingana na nadhiri aliyoweka, kadiri ya sheria ya kujiweka wakfu kwake.”

22. Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose,

23. “Mwambie Aroni na wanawe kwamba hivi ndivyo mtakavyowabariki Waisraeli: Mtawaambia,

24. ‘Mwenyezi-Mungu awabariki na kuwalinda;

25. Mwenyezi-Mungu awaangalie kwa wema, na kuwafadhili;

26. Mwenyezi-Mungu awaoneshe wema wake na kuwapa amani.’

27. “Ndivyo watakavyotamka jina langu juu ya Waisraeli, nami nitawabariki.”

Kusoma sura kamili Hesabu 6