Agano la Kale

Agano Jipya

Hesabu 5:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose,

2. “Waamuru Waisraeli wamtoe nje ya kambi kila mtu mwenye ukoma, kila mtu anayetokwa usaha, na kila aliye najisi kwa kugusa maiti.

3. Mtawatoa nje ya kambi watu wote hawa, wanaume kwa wanawake, ili wasije wakaitia najisi kambi yangu ninamokaa.”

4. Waisraeli walifanya hivyo, wakawafukuza nje ya kambi. Kama Mwenyezi-Mungu alivyomwambia Mose, ndivyo Waisraeli walivyofanya.

5. Kisha Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose,

6. “Waambie Waisraeli kuwa: Mtu yeyote, mwanamume au mwanamke akitenda dhambi dhidi ya mtu, akakosa uaminifu kwa Mwenyezi-Mungu, mtu huyo ana hatia;

7. itambidi aungame dhambi yake aliyotenda. Lazima atoe fidia kamilifu kwa kosa lake, akiongeza asilimia ishirini ya fidia hiyo; atampa fidia hiyo yule aliyemkosea.

8. Lakini ikiwa mtu huyo amefariki na hana jamaa wa karibu ambaye anaweza kupokea fidia hiyo, basi, fidia ya kosa itatolewa kwa Mwenyezi-Mungu kwa ajili ya makuhani; malipo haya ni pamoja na kondoo dume wa upatanisho ambaye atatumiwa kumfanyia upatanisho kwa ajili ya dhambi yake.

9. Michango yote na matoleo yote ambayo Waisraeli wataweka wakfu kwa Mungu na kumletea kuhani itakuwa yake huyo kuhani.

10. Kila kitu kilichowekwa wakfu kwa Mungu na kupelekwa kwa kuhani kitakuwa chake.”

Kusoma sura kamili Hesabu 5