Agano la Kale

Agano Jipya

Hesabu 32:1-14 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Makabila ya Reubeni na Gadi yalikuwa na mifugo mingi sana. Basi, walipoona kwamba eneo la Yazeri na Gadi lilifaa kwa mifugo,

2. waliwaendea Mose, kuhani Eleazari na viongozi wa jumuiya, wakawaambia,

3. “Miji ya Atarothi, Diboni, Yazeri, Nimra, Heshboni, Eleale, Sebamu, Nebo na Beoni,

4. nchi ambayo Mwenyezi-Mungu alishinda kwa ajili ya jumuiya ya Israeli, ni nchi nzuri kwa mifugo, nasi tunayo mifugo mingi sana.

5. Basi, kama mkitukubalia tunawaomba mtupe nchi hii iwe mali yetu; msituvushe ngambo ya mto Yordani.”

6. Mose akawajibu watu wa makabila ya Gadi na Reubeni, “Je, mnataka kubaki hapa huku ndugu zenu Waisraeli wanakwenda vitani?

7. Mbona mnawavunja moyo Waisraeli wasiende katika nchi ambayo Mwenyezi-Mungu amewapa?

8. Hivyo ndivyo walivyofanya babu zenu nilipowatuma kutoka Kadesh-barnea kuipeleleza nchi.

9. Wao walikwenda hadi bonde la Eshkoli, wakaiona nchi, lakini waliporudi, waliwavunja moyo Waisraeli ili wasiingie katika nchi aliyowapa Mwenyezi-Mungu.

10. Mwenyezi-Mungu aliwaka hasira siku hiyo, akaapa akisema,

11. ‘Hakika hakuna mtu yeyote kati ya watu waliotoka Misri mwenye umri wa miaka ishirini na zaidi atakayeiona nchi niliyoapa kuwapa Abrahamu, Isaka na Yakobo, kwa sababu hawakunitii kikamilifu.’

12. Wote hawataiona, isipokuwa Kalebu mwana wa Yefune, Mkenizi, na Yoshua mwana wa Nuni, maana wao wamenitii kikamilifu.

13. Mwenyezi-Mungu aliwaka hasira dhidi ya Waisraeli, akawafanya watangetange jangwani kwa muda wa miaka arubaini; kizazi kizima kilichokuwa kimefanya maovu mbele yake kikafariki.

14. Na sasa, enyi kizazi cha wenye dhambi, mmezuka mahali pa wazee wenu, kuongeza tena hasira kali ya Mwenyezi-Mungu dhidi ya Waisraeli.

Kusoma sura kamili Hesabu 32