Agano la Kale

Agano Jipya

Hesabu 31:19-32 Biblia Habari Njema (BHN)

19. Wote wale walio miongoni mwenu ambao wameua mtu au kugusa maiti ni lazima wakae nje ya kambi kwa muda wa siku saba; jitakaseni pamoja na mateka wenu katika siku ya tatu na ya saba.

20. Ni lazima mtakase pia kila vazi, kila kitu kilichotengenezwa kwa ngozi, kwa manyoya ya kondoo au kwa mti.”

21. Kuhani Eleazari akawaambia wanaume waliorudi vitani, “Hii ndiyo sheria ambayo Mwenyezi-Mungu amempa Mose.

22. Dhahabu, fedha, shaba, chuma, bati na madini ya risasi,

23. yaani vitu vyote ambavyo vinastahimili moto, vitatakaswa kwa kupitishwa motoni. Hata hivyo, ni lazima vitakaswe kwa maji ya utakaso. Vitu vingine vyote ambavyo haviwezi kustahimili moto vitatakaswa kwa maji ya utakaso.

24. Siku ya saba ni lazima muyafue mavazi yenu; ndipo mtakapokuwa safi na kuruhusiwa kuingia kambini.”

25. Mwenyezi-Mungu akaongea na Mose, akamwambia,

26. “Wewe na kuhani Eleazari, pamoja na viongozi wa koo za jumuiya ya Waisraeli, fanyeni hesabu ya nyara ya vitu, watu na wanyama.

27. Gaweni nyara katika mafungu mawili, fungu moja la wanajeshi waliokwenda vitani na fungu lingine kwa ajili ya jumuiya nzima.

28. Kisha kutokana na lile fungu la wanajeshi waliokwenda vitani, tenga zaka kwa ajili ya Mwenyezi-Mungu: Kitu kimoja kutoka kila vitu 500, iwe ni watu, ng'ombe, punda, kondoo au mbuzi,

29. umpe kuhani Eleazari kuwa sadaka kwa Mwenyezi-Mungu.

30. Kutoka lile fungu la jumuiya nzima, chukua sehemu moja ya kila hamsini, iwe ni watu, ng'ombe, punda, kondoo na mbuzi. Hivyo utawapa Walawi ambao wana wajibu wa kuhudumu katika hema la Mwenyezi-Mungu.”

31. Mose na kuhani Eleazari walifanya kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose.

32. Nyara walizoteka wanajeshi zilikuwa: Kondoo 675,000,

Kusoma sura kamili Hesabu 31