Agano la Kale

Agano Jipya

Hesabu 31:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Mwenyezi-Mungu aliongea na Mose, akamwambia,

2. “Walipize kisasi Wamidiani mambo waliyowatenda Waisraeli; kisha wewe utafariki.”

3. Basi Mose akazungumza na watu akawaambia, “Watayarisheni watu kwa vita waende kuwashambulia Wamidiani kumlipizia Mwenyezi-Mungu kisasi.

4. Kutoka kila kabila la Israeli, mtapeleka watu 1.000 vitani.”

5. Basi, watu 1,000 walitolewa kutoka kila kabila miongoni mwa maelfu ya Waisraeli, jumla wanaume 12,000 wenye silaha.

6. Mose aliwapeleka vitani chini ya uongozi wa Finehasi mwana wa kuhani Eleazari, akiwa na vyombo vya mahali patakatifu na tarumbeta za kutoa ishara.

7. Waliishambulia nchi ya Midiani, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose, wakawaua wanaume wote.

8. Miongoni mwa watu hao waliouawa, kulikuwako wafalme watano wa Midiani: Evi, Rekemu, Suri, Huri na Reba. Vilevile walimuua Balaamu mwana wa Beori.

9. Waisraeli waliteka nyara: Ng'ombe, kondoo na mali yao yote.

10. Miji yao yote, makazi yao na kambi zao zote waliziteketeza kwa moto.

11. Walichukua nyara zote na mateka yote, ya watu na ya wanyama,

12. wakampelekea Mose na Eleazari, na jumuiya yote ya Waisraeli iliyokuwa kambini katika nchi tambarare za Moabu, ngambo ya Yordani karibu na Yeriko.

Kusoma sura kamili Hesabu 31