Agano la Kale

Agano Jipya

Hesabu 28:9-27 Biblia Habari Njema (BHN)

9. “Siku ya Sabato, mtatoa sadaka ya wanakondoo wawili wa kiume wa mwaka mmoja wasio na dosari, sadaka ya nafaka ya kilo mbili za unga laini uliochanganywa na mafuta, na sadaka yake ya kinywaji.

10. Sadaka hii ya kuteketezwa itatolewa kila siku ya Sabato licha ya ile sadaka ya kila siku pamoja na sadaka yake ya kinywaji.

11. “Mwanzoni mwa kila mwezi, mtamtolea Mwenyezi-Mungu sadaka ya kuteketezwa: Fahali wadogo wawili, kondoo dume mmoja na, wanakondoo saba madume wa mwaka mmoja, wasio na dosari.

12. Mtatoa sadaka ya nafaka ya unga laini kilo tatu, uliochanganywa na mafuta kwa kila fahali mmoja; mtatoa kilo mbili za unga kwa kila kondoo dume,

13. na kilo moja ya unga kwa kila mwanakondoo. Sadaka hizi za kuteketezwa ni sadaka za chakula zenye harufu ya kumpendeza Mwenyezi-Mungu.

14. Kipimo cha sadaka ya kinywaji kinachohitajika ni lita 2 za divai kwa kila fahali; lita moja u nusu kwa kila kondoo dume, na lita moja kwa kila mwanakondoo. Hii ndiyo sadaka ya kuteketezwa ya kila mwezi katika mwaka mzima.

15. Tena mtamtolea Mwenyezi-Mungu sadaka ya kuondoa dhambi, beberu mmoja, licha ya ile sadaka ya kuteketezwa ya kila siku na sadaka yake ya kinywaji.

16. “Siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza ni Pasaka ya Mwenyezi-Mungu.

17. Siku ya kumi na tano ya mwezi huohuo ni sikukuu. Kwa muda wa siku saba mtakula mikate isiyotiwa chachu.

18. Katika siku ya kwanza kutakuwa na mkutano mtakatifu. Siku hiyo hamtafanya kazi.

19. Mtatoa sadaka ya kuteketezwa kama sadaka ya chakula kwa Mwenyezi-Mungu: Fahali wachanga wawili, kondoo dume mmoja, wanakondoo madume saba wa mwaka mmoja, wote wawe bila dosari.

20. Sadaka ya nafaka itakayoandamana nazo itakuwa ya unga safi uliochanganywa na mafuta, kilo tatu kwa kila fahali, kilo mbili kwa kila kondoo dume,

21. na kilo moja kwa kila mmoja wa wale wanakondoo saba.

22. Mtatoa pia beberu mmoja kuwa sadaka ya kuondoa dhambi ili kuwafanyia upatanisho.

23. Mtatoa vitu hivi licha ya ile sadaka ya kuteketezwa ya kawaida inayotolewa kila siku asubuhi.

24. Vivyo hivyo, kwa muda wa siku saba, mtatoa sadaka ya kuteketezwa ya kawaida ya chakula kwa kuteketezwa, ambayo ni harufu nzuri ya kumpendeza Mwenyezi-Mungu. Hii mtaitoa licha ya ile sadaka ya kuteketezwa ya kila siku na sadaka yake ya kinywaji.

25. Katika siku ya saba mtafanya mkutano mtakatifu; msifanye kazi.

26. “Mnamo siku ya kwanza ya sikukuu ya majuma wakati mnapomtolea Mwenyezi-Mungu malimbuko ya nafaka zenu, mtafanya mkutano mtakatifu; msifanye kazi.

27. Mtatoa sadaka ya kuteketezwa, harufu nzuri ya kumpendeza Mwenyezi-Mungu: Fahali wachanga wawili, kondoo dume mmoja, na wanakondoo saba madume wa mwaka mmoja, wote hao wawe hawana dosari.

Kusoma sura kamili Hesabu 28