Agano la Kale

Agano Jipya

Hesabu 25:7-18 Biblia Habari Njema (BHN)

7. Basi, Finehasi mwana wa Eleazari mwana wa kuhani Aroni alipoona hayo, aliinuka akatoka katika hiyo jumuiya, akachukua mkuki

8. na kumfuatia yule Mwisraeli mpaka hemani, akawachoma mkuki wote wawili tumboni. Maradhi mabaya yaliyokuwa yamewaangamiza Waisraeli yakakomeshwa.

9. Waliokufa kutokana na maradhi yale mabaya walikuwa watu 24,000.

10. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose,

11. “Finehasi mwana wa Eleazari, mwana wa kuhani Aroni, ameizuia hasira yangu dhidi ya Waisraeli; miongoni mwenu ni yeye tu aliyeona wivu kama nilio nao mimi. Ndio maana sikuwaangamiza Waisraeli wote kwa hasira yangu.

12. Kwa hiyo mwambie kwamba ninafanya naye agano la amani.

13. Naagana naye kwamba yeye na wazawa wake watakuwa makuhani milele kwa sababu aliona wivu kwa ajili yangu, Mungu wake, akawafanyia upatanisho Waisraeli.”

14. Huyo Mwisraeli aliyeuawa pamoja na mwanamke wa Kimidiani aliitwa Zimri mwana wa Salu, kiongozi wa jamaa mojawapo katika kabila la Simeoni.

15. Na huyo mwanamke Mmidiani aliyeuawa aliitwa Kozbi binti Suri, aliyekuwa kiongozi wa ukoo fulani huko Midiani.

16. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose,

17. “Wachokoze Wamidiani na kuwaangamiza,

18. kwa sababu waliwachokoza nyinyi kwa hila zao, wakawadanganya kuhusu jambo la Peori, na kwa sababu ya Kozbi, binti yao, aliyeuawa wakati maradhi mabaya yalipozuka kule Peori.”

Kusoma sura kamili Hesabu 25