Agano la Kale

Agano Jipya

Hesabu 22:1-8 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Waisraeli walianza safari tena, wakaenda kupiga kambi yao katika tambarare za Moabu, mashariki ya mto Yordani, kuelekea mji wa Yeriko.

2. Mfalme Balaki mwana wa Sipori, alijua mambo yote Waisraeli waliyowatendea Waamori.

3. Yeye pamoja na Wamoabu wakashikwa na hofu kubwa juu ya Waisraeli. Waliwaogopa hasa kwa sababu ya wingi wao.

4. Basi Wamoabu wakawaambia viongozi wa Midiani, “Umati huu punde si punde utaharibu kila kitu kandokando yetu kama fahali alavyo majani shambani.” Kwa hiyo, Balaki mwana wa Sipori, aliyekuwa mfalme wa Moabu wakati huo,

5. akapeleka ujumbe kwa Balaamu, mwana wa Beori, huko Pethori, karibu na mto Eufrate, nchini Amawi. Alimwambia Balaamu hivi: “Kuna taifa ambalo limetoka Misri, nalo limeenea kila mahali nchini, tena linatishia kuchukua ardhi yangu.

6. Njoo sasa uwalaani watu hawa kwa ajili yangu maana wana nguvu kuliko mimi. Labda nitaweza kuwashinda na kuwafukuza wasiingie katika nchi yangu, kwa maana najua kuwa wewe ukimbariki mtu hubarikiwa, ukimlaani mtu hulaaniwa.”

7. Basi, maofisa wa Moabu na Midiani wakachukua ada ya mwaguzi, wakaondoka kwenda kwa Balaamu. Walipowasili, walimpa Balaamu ujumbe wa Balaki.

8. Balaamu akawaambia, “Laleni huku usiku huu, nami nitawajulisheni atakayoniambia Mwenyezi-Mungu.” Basi, wazee hao wa Moabu wakakaa na Balaamu.

Kusoma sura kamili Hesabu 22